Na mwandishi wetu, Gazetini
WAKATI dunia ikiwa kwenye sintofahamu juu ya mustakabali wa vita vya Marekani na Iran, Kundi la kigaidi la Houthi nchini Yemen limeendelea kufanya mambo yawe mengi na magumu zaidi.
Iko hivi; Marekani na Iran zinaendelea kushambuliana na mgogoro wao juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz imesababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Hormuz ni njia muhimu ya maji kwani meli zinazobeba takribani asilimia 20 ya mafuta yanayoingia kwenye soko la dunia hupita hapo.
Hivyo, kutokana na mashambulizi yanayoendelea, ambapo Marekani na Iran zinagombea udhibiti wa njia hiyo, idadi ya meli zinazopita imepungua na kusababisha uhaba wa mafuta, hivyo kupanda kwa bei sokoni.
Sasa, wakati dunia ikibaki gizani juu ya lini vita vitakwisha ili bei ya nishati hiyo ishuke, Houthi imetangaza tishio la kuufunga Mlango-Bahari mwingine uitwao Bab al-Mandeb.
Kama ilivyo Hormuz, Bab al-Mandeb ni Mlango-Bahari mwingine muhimu katika usafirishaji wa mafuta duniani, ukitumiwa kupitisha asilimia kubwa ya meli zinazopeleka nishati hiyo barani Ulaya.
Kwa sasa, wapiganaji wa Houthi wanaudhibiti Mlango-Bahari huo na wamekuwa wakizishambulia meli zinazopita kupeleka mafuta Saudi Arabia, nchi inayoiunga mkono Serikali ya Yemen.
Houthi wanaoungwa mkono na mamlaka za Iran, wanaushikilia Mji Mkuu wa Yemen, Sanaa, tangu walipouteka mwaka 2014.
Hivi karibuni, Serikali ya nchi hiyo iliushambulia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa kwa madai kuwa ndege iliyokuwa imebeba viongozi wa Iran ilikuwa inajiandaa kutua hapo.
Licha ya Serikali kukiri kuhusika, Houthi walielekeza lawama kwa Saudi Arabia na kuishambulia, kabla ya kutangaza kuzuia meli zote zinazopita kupeleka mafuta katika nchi hiyo.
Serikali iliyoko madarakani nchini Yemen imekuwa ikiitegemea Saudi Arabia katika uendeshaji wa masuala nyeti ya kiusalama na kisiasa.


