Na mwandishi wetu, Gazetini
MWENYEKITI na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaji Aliko Dangote, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kutatua changamoto za uwekezaji nchini.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na makampuni ya Dangote katika maeneo ya nishati, viwanda, bandari, gesi, mbolea na miundombinu.
Katika hatua nyingine, Alhaji Dangote ameipongeza Serikali kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwamo kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili shughuli za Kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara.
Mfanyabishara huyo raia wa Nigeria, amesema jitihada hizo za Serikali zimeongeza tija na ufanisi wa uendeshaji, na imani ya kampuni hiyo kwa Tanzania kama eneo muhimu na la kimkakati la uwekezaji barani Afrika.
“Nataka nikushukuru kwa dhati kwa kushughulikia changamoto nyingi za uwekezaji wetu wa Kiwanda cha Saruji Mtwara. Ulipoingia madarakani tulikuwa na changamoto nyingi, lakini kama ulivyoahidi, kila changamoto imeshughulikiwa ipasavyo,” amesema
Wakati huo huo, Dangote Group tayari imeleta nchini malori 400 yanayotumia gesi asilia kwa ajili ya kusafirisha na kusambaza saruji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kubadilisha malori 700 ya kampuni hiyo kwenda katika matumizi ya nishati hiyo mbadala ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Alhaji Dangote amesema kiwanda hicho kinaendelea kufanya vizuri na kinatarajia kuzalisha takribani tani milioni 2.8 kwa mwaka huu, kati ya lengo lake la kuzalisha takribani tani milioni 3.2.

“Tunafanya vizuri. Lazima nikushukuru Mheshimiwa Rais kwa uongozi wako; kwa sababu bila uongozi wako, soko lisingekuwa bora na lenye tija ya kutuwezesha kufanya biashara kwa ukubwa huu,” ameeleza Alhaji Dangote.
Mazungumzo yao pia yameangazia uwezekano wa Dangote Group kuingia ubia na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mradi wa kusafisha mafuta ghafi unaokadiriwa kugharimu takribani Dola za Marekani bilioni 17, utakaonufaisha nchi za Afrika Mashariki na Ethiopia.
Alhaji Dangote amesema mradi huo unaweza kutoa fursa kwa nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki kushiriki kupitia umiliki wa hisa, kama sehemu ya kujenga uwezo wa Bara la Afrika katika kujitosheleza kwa uzalishaji wa mafuta na bidhaa za mafuta na hivyo kupunguza utegemezi kutoka nje na kujilinda dhidi ya athari za misukosuko ya bei na upatikanaji wa bidhaa hizo.
Kwa upande wake, Rais Dk. Samia amemhakikishia ushirikiano na amemuomba Alhaji Dangote kuendelea kuangalia fursa zaidi za biashara na uwekezaji nchini zenye tija na manufaa kwa mwekezaji, Serikali, na Taifa kwa ujumla.
Pia, Rais Dk. Samia ameikaribisha Dangote Group kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea nchini, akibainisha kuwa mahitaji ya bidhaa hiyo ni makubwa kuliko uwezo wa sasa wa uzalishaji wa ndani.



