Na Hassan Mwasha, Gazetini
SIMBA ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, haipaswi kupoteza hata mchezo mmoja, huku ikiiombea dua mbaya Yanga iliyoko kileleni mwa msimamo.
Wekundu wa Msimbazi wana pointi 52, wakati Yanga wana 54, huku kila timu ikiwa imashacheza mechi 23 kufikia hatua hii ya msimu wa 2025-26.
Katika michezo saba waliyonayo Simba, mitatu inaonekana kuwa ‘pasua kichwa’ zaidi kutokana na matokeo ya mzunguko wa kwanza dhidi ya timu hizo.
Mosi, kuna mechi yao dhidi ya Dodoma Jiji itakayochezwa Mei 24, 2026. Simba haikupata ushindi katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, na badala yake ilimazimishwa suluhu (0-0) ikiwa ugenini mjini Dodoma.
Pili, ni mechi dhidi ya Pamba Jiji, ambayo itachezwa Juni 14, 2026. Mchezo wa kwanza msimu huu wa Ligi ilichezwa Mwanza na Simba kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Tatu, mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa Juni 24, 2026, nayo si nyepesi kwa Wekundu wa Msimbazi. Timu hizo zilipokutana mzunguko wa kwanza, Simba ikiwa mwenyeji, zilitoka sare ya bao 1-1.
Kwa upande mwingine, pia Simba haipaswi kuzifumbia macho mechi dhidi ya Coastal Union (Mei 21, 2026) na Mbeya City (Juni 18, 2026) kwani ilizifunga ikiwa Dar es Salaam lakini sasa itazifuata kwenye viwanja vya mikoani.


