Na Hassan Mwasha, Gazetini
YANGA iko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 54, wakati Simba iko nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi mbili pekee, huku kila timu ikiwa imebakiza mechi saba kumaliza msimu.
Katika mechi saba zilizobaki, huenda presha ya mashabiki wa Yanga iko kwenye hizi mbili; dhidi ya Azam na TRA United. Kwanini? Ni timu ambazo mabingwa watetezi hao hawakuweza kuzifunga katika mzunguko wa kwanza.
YANGA V SINGIDA BLACK STARS
Katika mechi saba zilizobaki, Yanga itaanza na Singinda Black Stars, mchezo utakaochezwa Mei 22, 2026 kwenye Uwanja wa KMC. Mechi ya mzunguko wa kwanza ilimalizika kwa Singida iliyokuwa nyumbani kufungwa mabao 3-0.
YANGA V NAMUNGO
Hii ni mechi itakayochezwa Mei 25, 2026, ambapo Yanga watakuwa nyumbani katika Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam. Mechi ya mzunguko wa kwanza ilichezwa Lindi na Yanga kushinda bao 1-0.
MASHUJAA V YANGA
Mchezo ngumu kwa Yanga, ambayo itakuwa ugenini mkoani Kigoma. Mchezo huo utachezwa Juni 13, 2026, Mashujaa wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kutandikwa mabao 6-1 walipokutana na Yanga mzunguko wa kwanza.
FOUNTAIN GATE V YANGA
Mechi hii itachezwa Juni 17, 2026. Timu hizo zilipokutana katika mzunguko wa kwanza msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Yanga ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0. Je, Fountain watalipiza kisasi?
YANGA V AZAM
Safari hii, Yanga watakuwa nyumbani na mechi itachezwa Juni 24, 2026. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, timu hizo ziligawa pointi baada ya kutoka suluhu (0-0).
YANGA V TRA UNITED
Ni Juni 27, 2026, ambapo TRA United ya Tabora itaifuata Yanga katika Uwanja wa KMC. Mechi ya kwanza ilimalizika kwa TRA kulazimisha suluhu (0-0) mbele ya mabingwa watetezi hao.
JKT V YANGA
Hii ni mechi ya mwisho ya msimu huu wa Ligi Kuu. Yanga watakuwa ugenini kuwakabili ‘Maafande’ hao. Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, JKT hawakuweza kuzuia kipigo cha mabao 5-1.


