DAKAL, Senegal
BUNGE la Senegal limepitisha sheria mpya inayolenga kudhibiti tabia ya baadhi ya wabunge wanaosusia vikao vya Bunge bila sababu za msingi, hatua ambayo imeibua mjadala mkali wa kisiasa nchini humo.
Muswada huo ulipitishwa Ijumaa, Mei 8, 2026 kwa kura 127 dhidi ya tatu huku wabunge wawili wakijizuia kupiga kura. Sheria hiyo, iliyoungwa mkono na chama tawala cha PASTEF, inaweka adhabu kali zaidi kwa wabunge wanaokosa kuhudhuria vikao mara kwa mara bila udhuru.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo, mbunge ataanza kupewa onyo rasmi baada ya kukosa vikao vinne vya Bunge bila sababu, kabla ya kuchukuliwa hatua za kifedha ikiwemo kusimamishwa posho. Mbunge anayekosa vikao mara 10 bila sababu anaweza hata kupoteza kiti chake.
Kiongozi wa wabunge wa chama tawala cha PASTEF, Ayib Daffé, amesema sheria hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wabunge wanatimiza wajibu wao kwa wananchi waliowachagua.
“Hata kabla ya adhabu, mbunge ataombwa kujieleza kuhusu kutokuwepo kwake. Kuna ulinzi wa kutosha kuhakikisha haki inatendeka,” amesema Daffé.
Hata hivyo, upinzani umeipinga sheria hiyo ukidai inalenga kuwabana wabunge wenye misimamo tofauti. Mbunge wa chama cha PUR, Cheikh Ahmed Tidiane Youm, amesema suala la wabunge kutohudhuria vikao ni la kisiasa na halihitaji sheria mpya.
Naye mbunge mwingine wa upinzani, Thierno Alassane Sall, amesema Senegal ina changamoto kubwa zaidi zinazopaswa kupewa kipaumbele, ikiwemo deni la taifa na hali ya uchumi.
Mpaka sasa, Bunge la Senegal halijaweka wazi idadi ya wabunge wanaotuhumiwa kususia vikao mara kwa mara.


