8.9 C
New York

WWF yaongoza kampeni ya kuulinda mlima Kilimanjaro

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA jitihada za kulinda mustakabali wa mazingira na vyanzo vya maji, wadau wa mazingira wakishirikiana na jamii ya Moshi wameanzisha kampeni ya upandaji miti inayolenga kurejesha uoto wa asili unaozunguka Mlima Kilimanjaro.

Kupitia ushirikiano huo unaojumuisha Shirika la Kimataifa la Uhifadhi na Mazingira (WWF) pamoja na sekta binafsi, zaidi ya miti 3,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali yanayozunguka hifadhi hiyo maarufu duniani. Hatua hii inalenga kupunguza athari za ukame na kusaidia kuhifadhi mazingira ya mlima huo, ambao una umuhimu mkubwa kiikolojia na kiuchumi.

Shughuli hizo zimefanyika katika taasisi za elimu, ikiwemo shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Moshi, hatua inayolenga pia kuwajengea wanafunzi uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira tangu wakiwa wadogo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, mmoja wa washiriki kutoka WWF, Emmanuel Kivuyo, alisisitiza kuwa upandaji miti si tu hatua ya muda mfupi bali ni uwekezaji wa muda mrefu kwa ustawi wa mazingira.

Alieleza kuwa miti ina nafasi muhimu katika kulinda vyanzo vya maji na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo nyeti kama Mlima Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kivuyo, juhudi hizo ni sehemu ya mpango endelevu unaolenga kuhakikisha miti inayopandwa inalindwa na kukua ipasavyo, ili kuleta matokeo chanya kwa mazingira. Aliongeza kuwa hadi sasa, maeneo yenye ukubwa wa hekta 69 yameanza kunufaika na juhudi hizo kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo kampuni ya mawasiliano ya Yas.

Kwa upande wake, mwakilishi wa mazingira kutoka Manispaa ya Moshi, Stanley Jeremiah, alisema kuwa kampeni hiyo ya siku kadhaa imefanikiwa kupanda miti katika maeneo muhimu kama shule, hospitali na kando ya barabara.

Alibainisha kuwa juhudi hizo zinaendana na mkakati wa kitaifa wa kuimarisha uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na uharibifu wa misitu.

Naye Meneja Mahusiano wa kampuni ya Yas, Rukia Mtingwa, alieleza kuwa sekta binafsi ina jukumu muhimu katika kusaidia juhudi za uhifadhi wa mazingira. Alisema ushiriki wao unalenga kuhakikisha Mlima Kilimanjaro unaendelea kuwa kivutio cha utalii na chanzo cha ajira kwa jamii.

Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2024, zaidi ya miti 100,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kurejesha uoto wa asili uliopotea kutokana na shughuli za kibinadamu kama ukataji miti na uchomaji misitu.

Wadau hao wanaamini kuwa, pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, juhudi za pamoja kati ya taasisi, sekta binafsi na jamii zinaweza kurejesha uhai wa mazingira ya Kilimanjaro na kulinda rasilimali zake kwa vizazi vijavyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img