9.5 C
New York

JET: Wanawake wana wajibu wa kuhifadhi mazingira

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimetoa wito kwa wanawake nchini kuendelea kubeba wajibu wa kuiongoza jamii katika kuhifadhi mazingira ya asili.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Machi 7, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, John Chikomo, amesema mwanamke ni nguzo ya uhai na malezi, hivyo utunzaji wake wa mazingira ni ulinzi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema wanawake wana wajibu wa kuhamasisha jamii kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji na kupunguza taka ili kutengeneza mazingira safi na endelevu.

“Katika kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8, 2026, JET inasisitiza heshima kwa wanawake na kuwaomba kuendelea kutunza mazingira ya asili kwani wana wajibu wa kuongoza jamii katika kuyahifadhi,” amesema Chikomo.

Ujumuishwaji katika sheria

Chikomo amesema jitihada za kuleta usawa wa kijinsia katika masuala mbalimbali nchini zinaonyesha mabadiliko makubwa ya kimaendeleo, hususan katika upatikanaji wa haki za wanawake katika usimamizi wa rasilimali.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025, Serikali ya Tanzania ilichukua hatua za makusudi kuimarisha hadhi ya kisheria ya wanawake katika umiliki wa ardhi.

“Sera ya Taifa ya Ardhi iliyorekebishwa (toleo la 2023), iliyozinduliwa rasmi Machi 2025, inathibitisha haki sawa kwa wanawake kupata, kumiliki na kurithi ardhi, pamoja na kushiriki katika mipango ya uhamasishaji wa umma kuhusu matumizi endelevu ya ardhi,” amesema.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inawapa wanawake nafasi kubwa ya kuwa vinara katika kulinda na kuhifadhi mazingira, huku wakiwa na jukumu la kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa maliasili.

Chikomo amesema takwimu za kitaifa zinaonyesha maendeleo yanayopimika, ambapo wanawake sasa wanamiliki takriban asilimia 34 ya ardhi ikilinganishwa na asilimia 37 ya wanaume, hali inayoonyesha kupungua kwa pengo la kijinsia.

Aidha, amesema mipango ya uthibitishaji wa ardhi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali na washirika wa maendeleo imesaidia kuongeza idadi ya vyeti vya ardhi vinavyotolewa kwa wanawake, ambapo katika baadhi ya wilaya karibu asilimia 45 ya vyeti hivyo vimetolewa kwa wanawake.

Amesema hatua hizo zinaongeza usalama wa umiliki wa ardhi kwa wanawake na kuimarisha uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za ardhi.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, JET imeendelea kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa maliasili kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana wote, ikiwa ni pamoja na kukuza mifumo ya kisheria iliyo na usawa na jumuishi, kuondoa sheria, sera na desturi za kibaguzi pamoja na kushughulikia vikwazo vya kimuundo vinavyokwamisha maendeleo yao.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img