Na mwandishi wetu, Gazetini
MIAKA ya hivi karibuni imeshuhudia migogoro mingi ya wanamuziki wa Bongo Fleva na mabosi wa lebo zao.
Mfano wa hivi karibuni ni hiki kinachoendelea sasa kati ya msanii Mac Voice na lebo ya Next Level inayomilikiwa na staa Rayvanny.
Mambo yamekuwa mengi, huku Mac Voice akilalama kupitia vituo vya redio na runinga kwa kile anachodai kutokutendewa haki akiwa chini ya lebo hiyo.
Nimebahatika kumsikiliza katika moja ya mahojiano, ambapo Mac Voice alifichua hali mbaya ya maisha aliyopitia akiwa hapo.
Machache kati ya mengi aliyosema ni pamoja na kulala studio na kunyimwa fedha alizomuomba Rayvanny kwa ajili ya matibabu ya mama yake.
Ni ngumu kugusa kila alichosema Mac Voice lakini madai yake hayo yanaendeleza kile kinachotosha kusema lebo za muziki zimegeuka ‘jehanamu’ kwa wasanii wa Bongo Fleva.
Tofauti na miaka mingi iliyopita, ambapo ilikuwa moja ya ndoto za mafanikio kwa msanii, kwa sasa lebo si mahala salama tena.
Tujikumbushe; kabla ya hiki kinachoendelea kati ya Mac Voice na Rayvanny, kuna orodha ndefu ya wasanii waliokimbia lebo zao katika mazingira ya aina hii.
Kama inafaa kukumbusha, hilo lilitokea wakati Angela alipoondoka Konde Gang, Lebo inayomilikiwa na supastaa wa Bongo Fleva, Harmonize.
Kumbuka pia madai ya akina Kiri walivyoondoka katika Lebo ya Kings Music ya msanii mwingine maarufu, Ali Kiba.
Kama hiyo haitoshi, vipi kuhusu mgogoro wa Harmonize na Rich Mavoko walivyoondoka Wasafi Classic Baby (WCB) ya Diamond Platinumz. Ni kwa nyakati tofauti lakini kwa mazingira haya haya ya migogoro.
Nini chanzo?
Licha ya kila mmoja kuwa na sababu zake, wengi huangukia katika maeneo mawili. Ni yapi hayo?
Mosi, matarajio kutofikia uhalisia. Kwamba msanii anaposainiwa na Lebo kama Kings Music, Konde Gang au WCB, matarajio yake huwa ni makubwa.
Huamini kuwa kazi zake ‘zitatembea’ zaidi, labda mara mbili au tatu ya alivyokuwa peke yake. Mambo yanapokwenda tofauti, huanza kupoteza imani na mahala alipo, hivyo kutamani kutoka.
Pili, kuna shida ya menejimenti katika lebo. Huenda wamiliki wa lebo hudhani fedha pekee zinatosha, na mwishowe kupuuza umuhimu wa elimu ya namna ya kusimamia wasanii.
Kwa nyakati tofauti katika madai yao, wengi kati ya wasanii walioondoka WCB, Kings Music na Konde Gang, ishu ya kukosekana mfumo mzuri wa mawasiliano ndani ya taasisi hizo imeonekana kwa kiasi kikubwa.
Mathalan, hebu turudi kwa Mac Voice alipoomba asaidiwe fedha za matibabu ya mama yake. Huenda ni kweli Rayvanny au Lebo haikuwa na fedha.
Lakini, kama kungekuwa na mfumo rafiki wa kuwasilisha taarifa hiyo kwa Mac Voice, basi ‘dogo’ angechukulia poa na kujihisi bado ni sehemu ya familia. Maisha yangeendelea.
Hata ukirudi kwa wengine, utabaini kuwa hawakuwa na mawasiliano mazuri na mabosi wa lebo hata miezi miwili hadi mitatu kabla ya kuvunja ukimya na kuondoka.
Basata nayo kikaangoni
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limekuwa likipewa heshima ya ‘mzazi’ ndani ya Bongo Fleva. Migogoro mingi ya hivi karibuni kati ya wasanii na Lebo zao imekuwa ikipelekwa hapo.
Cha kushangaza, ni kile alichokisema Mac Voice, kwamba alipopeleka suala lake pale, alizungushwa kwa muda mrefu bila kupatiwa msaada.
Hata alipokutana na mkubwa, ambaye amemtaja kwa jina katika mahojiano, bado majibu yalikuwa ya kukatisha tamaa zaidi.
Kwa mujibu wake, bosi akasema hawezi hawezi kushughulikia sakata hilo kwa kuwa yeye na Rayvanny ni marafiki wakubwa. Akamtaka Mac Voice arudi akamalizane na Rayvanny.
Chukulia mfano; umekwenda kituo cha polisi kumshitaki mwizi wako, halafu pale unaambiwa ‘huyo mwizi ni rafiki yetu, hatuwezi kumkamata, rudi nyumbani mkamalizane’.
Nikirudi kwa BASATA, kilichofanywa na huyu bosi ni ishara kwamba Taasisi hiyo imewagawa wasanii. Kwamba wapo wenye nguvu ya kuumiza wenzao kutokana na ushawishi na urafiki wao na wakubwa.
Hatima yake ni nini? Huenda kwa staili hii tusishuhudie tena kesi nyingi za aina hii zikienda BASATA. Labda tutaanza kushuhudia wasanii ‘wakimalizana’ wenyewe huko mitaani, jambo linaloweza kusababisha hatari zaidi.


