LOS ANGELES, Marekani
HATIMAYE mama mzazi wa rapa Nicki Minaj, Carol Maraj, amefuta kesi baada ya mtu aliyemuua mumewe kukubali kulipa fidia ya Dola za Marekani 400,000 (zaidi ya Tsh bilioni moja za Tanzania).

Baba yake Minaj, Robert Maraj, alifariki mwaka 2021 kwa kugongwa na gari na mwanaume anayefahamika kwa jina la Charles Polevich.
Mbali ya Dola 400,000, pia familia ya Minaj italipwa kiasi kingine cha fedha kinachotajwa kuwa ni Dola 100,000 kutoka kwa kampuni ya bima.
Kwa wasiomfahamu, Maraj na mkewe, Carol, walimpata Minaj wakiwa wanaishi nchini Trinidad, wakati huo wakiwa wamempa jina la Onika Tanya Maraj.
Minaj akiwa na umri wa miaka mitatu, alibaki Trinidad akiwa na bibi baada ya wazazi wake kuhamia New York, Marekani.
Miaka miwili tu baadaye, wazazi walirejea na kumchukua Minaj, pamoja na kaka yake, safari hii wakihamia Jamaica.
Wakati Minaj anakua, mzee wake, Maraj, alijikuta kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Minaj amewahi kusimulia namna mzee wake huyo alivyoweza hata kuiba vitu ndani ili tu kupata pesa za kununua cocaine.
Miaka mingi baadaye, kwa mujibu wa Minaj, baba yake alibadilika na kuacha ‘unga’, na wakati mwingine kwenda kanisani.
Februari, 2021, Maraj alipoteza maisha baada ya kugongwa na gari na mtu ambaye hata hivyo alikimbia, kabla ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja, adhabu ambayo Carol aliikatia rufaa akisema ni ndogo dhidi ya mtu aliyemuua mumewe.


