22.1 C
New York

Maisha, utata wa kifo, maziko ya Rais Edgar Lungu (2)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA toleo la kwanza lililopita, tuliona Lungu akikaimu urais baada ya Michael Sata kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Ni kuanzia mwaka 2013 hadi 2014.

Pia, tukaona kifo cha Sata kilichotokea Oktoba 28, 2014, na nafasi yake ya urais kushikiliwa kwa muda na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Guy Scott.

Wakati ukisubiriwa Uchaguzi mdogo wa kuziba pengo la Sata, tuligusia Lungu akipewa nafasi kubwa kwa sababu Dkt. Scott asingeweza kuwa Rais kwa sababu wazazi wake hawakuzaliwa Zambia. Endelea na makala.

Januari 20, 2015, Lungu akiwa Rais wa Chama cha PF, aligombea kiti cha urais katika Uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya Sata, ambapo alimshinda mgombea wa Chama cha upinzani cha United Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema.

Katika mabadiliko yake ya mapema, alimteua Inonge Wina kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Makamu we Rais nchini humo.

Miezi miwili baadaye, Lungu alikuwa hospitali huko Afrika Kusini baada ya kuangukia akiwa jukwaani wakati wa hotuba yake kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mjini Lusaka.

Aliporejea, alitoa msamaha kwa wafungwa 332 waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha, pia akikosoa hali mbaya katika Gereza la Mukobeko.

Baadaye, Lungu aliitangaza Oktoba 18, 2015 kuwa Siku Maalum ya Kitaifa ya kuiombea hali mbaya ya kiuchumi, ambapo viongozi wa dini, sambamba na wanasiasa, walishiriki.

Licha ya jitihada kubwa za kuinua uchumi, hasa katika kuiondoa Zambia katika utegemezi wa madini ya shaba, na badala yake kuweka nguvu kwenye sekta zingine, Lungu hakuepuka kukosolewa.

Wakosoaji wake hawakufurahishwa na namna utawala wake wa mwaka mmoja (2015-16) ulivyobana uhuru wa vyombo vya habari.

Alipomaliza awamu ya Sata, Lungu aligombea muhula wake kamili kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, ambapo alikutana tena na Hichilema wa UPND, kama ilivyokuwa mwaka 2015.

Safari hii, Lungu alishinda kiti cha urais kwa asilimia 50.32 lakini Hichilema alipinga matokeo mahakamani akisema ulitawaliwa na ‘ujanjaujanja’.

Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali madai hayo na hatimaye Lungu aliapishwa kuwa Rais mpya Septemba 13, 2016.

Mwaka 2019, Lungu alitoa msimamo mkali juu ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, akisema haviwezi kukubalika kwa kuwa ‘hata wanyama hawafanyi hivyo’.

Mwaka 2021, katika Uchaguzi Mkuu uliofuata, Lungu alijitosa tena kuwania urais, akisaka muhula wake wa pili, ukiacha miezi kadhaa aliyomalizia utawala wa Sata.

Kwa mara ya tatu, alikutana tena na Hichilema na safari hii ni Lungu ndiye aliyepoteza akizidiwa kura takribani milioni moja.

Tofauti na ilivyokuwa kwa Hichilema katika chaguzi zilizopita, Lungu alikubali matokeo na mpinzani wake huyo akaapishwa kuwa Rais wa Zambia.

Ni baada ya matokeo hayo, Lungu akatangaza rasmi kuachana na siasa za ushindani na kuachia ngazi katika nafasi yake ya Rais wa Chama cha PF.

Je, nini kilifuata katika maisha yake ya nje ya siasa? Usikose sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala haya ya maisha,   utata wa kifo na maziko ya Rais Edgar Lungu.

Related articles

Recent articles