4.3 C
New York

Jay Z; Kutoka ‘uswazi’, kukimbizana na polisi hadi bilionea wa Hip hop

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

NI rahisi kuona watu wakikuwekea chuki na wivu kwa vile tu umefanikiwa, bila kujua umepitia shida nyingi kufika hapo ulipo. Wanachukulia poa tu!

Akiwa hana baba, pesa wala tumaini, hakuna aliyejua kama leo hii kinana wa mitaa ya Brooklyn angekuwa staa na bilionea mkubwa nchini Marekani na duniani kwa ujumla.

Huyo ndiye Jay Z, mwanamuziki wa kwanza wa Hip hop kuwa na hadhi ya kuitwa bilionea.

Jina lake halisi ni Shawn Corey Carter na alizaliwa mwaka 1969 mjini Brooklyn, New York.

Alipokuwa na umri wa miaka 11, alipoteza uwepo wa baba. Mzee alikimbia familia na kumwachia mama aitwaye Gloria mzigo wa kulea watoto wanne.

Katika mtaa walioishi, uhalifu ulitamalaki kwa kiwango cha kutisha, kiasi cha milioni ya risasi za polisi kuwa ni kitu cha kawaida tu.

Dawa za kulevya ziliuzwa kama pipi dukani, hivyo haikushangaza kuona Jay Z naye akijitosa kuuza cocaine ili kumsaidia majukumu ‘bi mkubwa’ wake huyo. Wakati huo akiwa na miaka 12 tu.

Tukio la kukumbukwa zaidi wakati huo ni lile la Jay Z kumpiga risasi kaka yake walipotibuana katika biashara ya kuuza ‘unga’.

Tofauti na wenzake, Jay Z alionesha upekee wake wa namna ya kutunga na kuimba mashairi ya Hip hop akiwa kwenye mizunguko yake.

Baada ya lebo nyingi kumkataa, Jay Z alianzisha yake mwenyewe akiwa na umri wa miaka 26 tu. Akaiita Roc-A-Fella Records.

Mwaka 1996, Jay Z aliushtua ulimwengu wa Hip hop alipoachia albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la ‘Reasonable Doubt’.

Alipoachia albamu ya pili, ‘The Blueprint’ mwaka 2001, ambayo iliuza nakala 427,000 katika wiki ya kwanza tu, Jay Z akawa hashikiki tena.

Hata hivyo, tofauti yake na wasanii wengine wa Hip hop ni jicho zuri la kibiashara alilonalo Jay Z.

Aliuza lebo yake ya Roc-A-Fella Records kwa Def Jam, dili lililompa mkwanja mrefu (Dola milioni 10). Baadaye, akawa ndiye Rais wa Def Jam.

Alianzisha kampuni ya mavazi ya Rocawear na kisha kuiuza kwa Dola milioni 204.

Mbali ya biashara zingine, Jay Z ni mmiliki wa kampuni ya uwakala wa michezo ya Roc Nation Sports.

Pia, aliingia Dola milioni 630 kwa kuuza asilimia 50 ya hisa katika Kampuni ya LVMH, ambayo inajihusisha na bidhaa mbalimbali za bei kubwa duniani.

Vilevile, Jay Z ni mmiliki wa kampuni ya muziki ya Tidal, wakati huo huo akiwa amewekeza katika sekta ya usafirishaji kupitia hisa zake katika kampuni Uber.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img