BEIJING, China
LICHA ya umri wake wa miaka 101, Jiang Yueqin haonekani ni mtu mwenye afya iliiyodhohofika. Bado ana meno yake yote 32 na amekuwa akitumia muda mwingi kutazama runinga sebuleni kwake.
Yueqin, mkazi wa Mji wa Wenzhou ulioko Mashariki mwa China, anasema huwa anakula mara mbili kwa siku, ingawa wakati mwingine huamka usiku na kupata ‘cha kutafuna’ pale anapohisi njaa.
Akihojiwa na Gazeti la mtandaoni la Daily Mail la Uingereza, anasema muda wake wa kulala ni usiku wa saa 8 na siku zote huamka saa 4 asubuhi.
Anapoamka, tofauti na watu wengi, hula kwa pamoja kifungua kinywa (chai ya rangi) na chakula cha mchana, kisha kusubiri mlo wa pili ifikapo saa 12 jioni.
Siku yake huanza kwa kikombe cha chai ya rangi, kabla ya kuvaa na kupata mlo wa asubuhi, na kisha chakula cha mchana ifikapo saa 6 mchana.
Binti yake aitwaye Yao Songping ni shuhuda mzuri wa namna mama yake alivyo ‘fiti’, licha ya umri mkubwa alionao. Anasema: “Mama yangu ni kama kijana, inashangaza sana.
“Anachelewa sana kulala lakini ataamka saa 4 asubuhi kama watu wengine. Huwa anakula kwa pamoja chai na chakula cha mchana. Kama atahisi njaa usiku, basi atakula vitu vya kutafuna tu.”
Songping anafichua kuwa baba yao alifariki miaka mingi iliyopita. Kwa mujibu wa majirani, Yueqin na mumewe walikuwa ni watu wanaopendana mno.
Akizungumzia hilo, Songping anasema: “Mama yangu hajui kusoma wala kuandika. Hivyo, baba ndiye aliyekuwa akimsomea.
“Jambo la kwanza ambalo baba angefanya baada ya kupokea mshahara ni kununua tiketi ya kwenda kutazama sinema na kwenda na mama.”
Aidha, Songping anasema bado mama yake, licha ya ukongwe alionao, amekuwa akikumbushia nyakati nzuri alizokuwa na mumewe.
Katika kumuondoshea upweke, watoto wake saba wamekuwa wakiambatana naye kusafiri maeneo mbalimbali nchini China.
Kwa miaka miwili iliyopita, ajuza huyo alitembelea miji zaidi ya 20, ikiwamo Dongtou, Yongjia, Jinhua na Suzhou.
Mwaka jana, mkazi wa Newbury, Barbra Evans, alifariki akiwa na umri wa miaka 103. Aliwahi kusema: “Siri ya kuishi miaka mingi ni kutokuiga maisha ya wengine na kusema ukweli.”


