KIGALI, Rwanda
KWA miaka ya hivi karibuni, Rwanda imewekeza vya kutosha katika kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi, takwimu zinaeleza.
Kwa mwaka 2024, maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yalikuwa ni 2,555, tofauti na 2,922 kwa takwimu za mwaka 2023.
Kwa takwimu zilizotolewa na Serikali mwaka jana, kushuka kwa idadi ya maambukizi mapya kumeshuhudiwa katika majimbo yote nchini humo.
Je, nini siri ya mafanikio hayo? Ofisa wa Mfuko wa Ukimwi nchini Rwanda (AHF), Dk. Gilbert Mbaraga, anasema:
“Rwanda imepiga hatua kubwa ya kupunguza maambukizi mapya kutokana na uwepo wa programu za kitaifa, ambapo mamlaka zimekuwa zikifuatilia watu walioathirika.
“Zimekuwa zikifuatilia wenza wao, ndugu zao na hata watu wao wengine wa karibu kupitia programu inayoitwa ‘index testing’. Tunafuatilia walioathirika na watu wanaoweza kuwaambukiza. Programu hii imekuwa na matokeo mazuri sana nchini,” anasema.
Pia, Dkt. Mbaraga anafichua namna wanawake wajawazito wanavyofuatiliwa juu ya hali yao ya afya hata miaka miwili baada ya kujifungua.
“Kwa upande wa vijana, tukitambua kundi hilo lilivyo hatarini zaidi, tuna vituo vya elimu ya Ukimwi na afya ya uzazi katika maeneo mengi nchini.
“Elimu ya matumizi sahihi ya kondomu, hasa katika taasisi za elimu ya juu, ni sehemu muhimu ya jitihada tunazofanya,” anasisitiza.
Naye Katibu Mkuu wa Mtandao wa Watu Wanaoishi na Ugonjwa huo nchini humo (RRP+), Deo Mutambuka, anaongeza:
“Takwimu zinaonesha hatua kubwa iliyopigwa katika upatikanaji wa huduma za Ukimwi na afya ya uzazi kwa ujumla wake katika miaka ya hivi karibuni.”
Mtaalamu huyo, Mutambuka, anasema mamlaka zimefanya kazi kubwa ya kusambaza vituo vya afya katika maeneo mengi nchini humo. “Hii imerahisisha matibabu, hasa kwa watu wa vijijini,” anasema.
Kwa upande mwingine, Mutambuka anaeleza kuwa jitihada kubwa ya kuondosha dhana ya unyanyapaa nayo imehamasisha watu kupima na kufahamu hali ya afya zao mapema na kuanza matibabu.
“Tumeanza kuona watu wenye Ukimwi sasa wakishiikiana kwa kufuatiliana na hata kutembeleana hadi nyumbani,” amesema Mutambuka.
Wakati huo huo, Mutambuka anaeleza nafasi kubwa ya Mtandao wake wa RRP+ katika mafanikio iliyoyapata Rwanda katika vita dhidi ya Ukimwi.
“RRP+ inafanya kazi kuanzia chini, wilaya, majimbo na hata ngazi ya taifa. Mtandao unaendesha mafunzo kwa taasisi zingine zaidi ya 5,000 nchi nzima,” anasema Mutambuka.
Wakati huo huo, Mutambuka anasisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili Rwanda kuweza kupunguza zaidi, kama si kumaliza kabisa, maambukizi ya Ukimwi.
Kwa upande wake, elimu inapaswa kuelekezwa zaidi kwa kundi la vijana. “Kwa vijana wengi, kujikinga na ujauzito ni kipaumbele zaidi, kuliko Ukimwi. Kujikinga na Ukimwi kunapaswa kuwa msingi wa elimu ya uzazi,” anasema.
Naye Mratibu wa Programu za Afya katika Shirikisho la Sekta Binafsi nchini Rwanda, Leon Pierre Rusanganwa, anasema vitendo vya unyanyapaa bado ni changamoto inayokinzana na vita dhidi ya Ukimwi.
“Unyanyapaa na ubaguzi bado ni changamoto. Kwa sababu kama watu hawajitokezi na kupima kwa hiyari, ni ngumu kwao kujua afya zao na kuanza matibabu. Kama hakuna matibabu, ni rahisi kwa ugonjwa kusababisha vifo,” anaongeza.


