Na mwandishi wetu, Gazetini
SPIKA wa Bunge la Wawakilishi la Australia, Milton Dick, amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika Mkutano wa 153 wa Umoja huo unaofanyika Arusha, Tanzania.
Dick amepata asilimia 56 ya kura katika upigaji kura wa siri uliofanyika kwa awamu moja, akimrithi Dkt. Tulia Ackson wa Tanzania, aliyemaliza muhula wake wa miaka mitatu katika nafasi hiyo.
Dick ni Mbunge wa jimbo la Oxley, Queensland, tangu mwaka 2016. Alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Wawakilishi la Australia kwa mara ya kwanza mwaka 2022 na kuchaguliwa tena bila kupingwa mwaka 2025.
Katika shughuli zake za kibunge, amejikita katika kusimamia haki na kutopendelea upande wowote, ushirikishwaji, diplomasia ya kibunge na kujenga mazingira salama na yenye kuheshimiana mahali pa kazi.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Dick amesisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano, akisema uchaguzi huo haupaswi kutafsiriwa kuwa kuna washindi na walioshindwa, bali ni ishara ya demokrasia na sauti ya pamoja ya IPU.
“Leo hakuna washindi wala walioshindwa. IPU imezungumza kwa sauti moja. Hii ndiyo demokrasia.
“Ni ukumbusho kwamba mazungumzo bado yana umuhimu, heshima bado ina umuhimu na ushirikiano bado una umuhimu. Tutafanya kazi pamoja, tutasikilizana na tutatafuta maeneo tunayokubaliana,” amesema Dick.
Katika nafasi hiyo mpya, Dick ataongoza mikutano rasmi ya IPU na kuiwakilisha taasisi hiyo katika matukio makubwa ya kimataifa, akishirikiana kwa karibu na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Anda Filip.
Uchaguzi wake unafungua ukurasa mpya kwa IPU, wakati wabunge kutoka mataifa mbalimbali wakiendelea kuimarisha mazungumzo, uwakilishi wa kidemokrasia na ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili dunia.


