Na Faraja Mulungu, Gazetini- Moshi
“CHANGAMOTO ni kwamba bei bado si rafiki. Wananufaika zaidi wakusanyaji, na sisi hatuyajui masoko mengine. Kwa hiyo tunakubali wanachotupa kwa sababu tunajua hatuna mitaji mikubwa.”
Hiyo ni kauli ya Mashaka Innocent, mchinjaji wa ng’ombe wa mkoani Geita, akielezea changamoto zinazowakabili katika biashara ya ngozi za mifugo, licha ya bidhaa hiyo kuwa na thamani katika mnyororo wa uzalishaji wa viwanda vya ngozi.
Kwa kawaida, thamani ya ng’ombe huanza kujidhihirisha akiwa hai, kupitia uzalishaji wa maziwa yanayotumika kama chakula na malighafi ya kutengeneza bidhaa mbalimbali na samadi ambayo hutumika kama mbolea ya asili katika kilimo, pamoja na kuzalisha gesi asilia (biogas) inayoweza kutumika kwa kupikia na kuzalisha nishati ya umeme.
Kwa upande wa pili ng’ombe anapochinjwa, huendelea kuwa chanzo cha thamani ya kiuchumi kupitia nyama inayotumika kwa chakula na biashara, huku sehemu nyingine za mwili wake zikitoa malighafi kwa matumizi mbalimbali ya viwandani.

Ngozi ambayo hubaki baada ya uchinjaji ni rasilimali nyingine yenye thamani kiuchumi kikiwa chanzo cha ziada cha mapato katika mnyororo wa thamani; pale ambapo hukusanywa, kuhifadhiwa, kusindikwa na kuongezewa thamani kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama vile viatu, mikanda, mikoba na bidhaa nyingine za ngozi.
Hii ndiyo fursa inayobebwa na Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited – KLICL), kilichopo Karanga, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, pembezoni mwa Barabara ya Moshi–Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa KLICL, Abednego Aligawesa anasema kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake unafikia Sh bilioni 152.96 ni fursa kwa wafugaji kuuza ngozi za mifugo; ng’ombe, mbuzi na kondoo ambazo hutumika kama malighafi kuu ya kutengenezea bidhaa.
Uwekezaji huo unjumuisha viwanda vinne vinavyohusisha usindikaji wa ngozi, utengenezaji wa viatu, uzalishaji wa soli na bidhaa nyingine za ngozi kama mikoba, mikanda na makoti.
“Tunazalisha ngozi, jina linalojulikana ni ngozi, lakini ile ngozi sasa na yenyewe inakuwa na saizi na vipimo vyake kulingana na mtu (mteja) unahitaji ngozi au bidhaa za aina gani, kwa hiyo ikitokea mteja ameleta mapendekezo yake mfano viatu vya kung’aa au kufuata, tunazalisha,” anasema Aligawesa.
Kampuni ya KLICL ilianzishwa Mei 26, 2017, kupitia ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) waanaomiliki asilimia 86 ya hisa na Jeshi la Magereza kupitia Prisons Corporation Sole (PCS) wanaomiliki asilimia 14. Kabla ya kuundwa upya, awali KLICL ilijulikana kama Karanga Leather Industries Company Ltd.
Kwa sasa, KLICL ina wafanyakazi wapatao 300, idadi inayotarajiwa kuongezeka kadiri shughuli za uzalishaji zitakavyopanuka na kufikia lengo la kuajiri watu 3,000, kuaji unategemea pia uwezo wa kiwanda kuongeza uzalishaji, kupanua masoko na wateja wa bidhaa zake.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina zaidi ya ng’ombe milioni 40.7, hivyo sekta ya ngozi ina nafasi kubwa ya kuchochea uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Malighafi na uzalishaji
Meneja Uzalishaji wa KLICL, Saiba Edward, anasema kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika ngozi za ng’ombe milioni 1.8 kwa mwaka na ngozi za mbuzi na kondoo milioni 4.32. Pia kina uwezo wa kuzalisha jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka, kikiwa na mitambo ya kutengeneza soli na bidhaa nyingine za ngozi.
Hata hivyo Hotuba ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya 2026/27, inaonyesha kuwa katika wa mwaka wa fedha 2025/2026 kiwanda kilisindika ngozi 360,000 za ng’ombe, sawa na takribani asilimia 20 ya uwezo wake, na ngozi 85,000 za mbuzi na kondoo, kiwango kilicho chini ya asilimia mbili ya uwezo uliokusudiwa.
Wakati takwimu hizo zikiashiria upungufu wa malighafi kiwandani, hali halisi katika baadhi ya maeneo nchini inaonesha kuwawepo kwa ngozi, hali inayoashiria kuwa changamoto kukosekana kwa taarifa za uwepo wa soko kwa wafugaji na wadau wengine wanaozalisha malighafi hiyo.
Mfano hai ni mkoani Geita ambako Mwenyekiti wa Wafugaji Kanda ya Ziwa, Tryphone Kambona, anasema wafugaji wengi hawafahamu uwepo wa fursa ya soko la ngozi wala manufaa wanayoweza kuyapata kupitia zao hilo. Hata hivyo, tofauti na wafugaji hao, wachinjaji katika mkoa huo wamekuwa wakishiriki katika biashara ya ngozi kupitia mawakala kwa zaidi ya miaka 10.
Kambona anasema uwepo wa kiwanda cha ngozi ni fursa muhimu kwa sekta ya mifugo, lakini taarifa kuhusu kiwanda hicho na namna wafugaji wanavyoweza kunufaika nacho hazijawafikia wengi, ambao wamejikita zaidi katika ufugaji wa kunenepesha na ule wa asili.
“Kwa mwaka mmoja ambao nimekaa kwenye nafasi hii, sina taarifa kuhusu kiwanda cha ngozi ambacho kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwetu. Sisi tunafanya ufugaji wa kunenepesha na ufugaji wa asili,” anasema Kambona.
Anasema hali hiyo inaonesha umuhimu wa kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu thamani ya ngozi na nafasi yao katika mnyororo wa biashara hiyo. Wafugaji wengi wanapouza ng’ombe hawafuatilii hatima ya ngozi baada ya mnyama kuchinjwa, hivyo kukosa fursa ya kunufaika na zao hilo.
Kwa upande wake Mfugaji Maduhu Pongwa wa mkoani Simiyu anasema uwepo wa soko la uhakika la ngozi unaweza kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafugaji. “Wengi wetu huwa tunamini kuwa nyama pekee ndiyo kitu cha msingi, labda na maziwa na mbolea wakati mwingine. Lakini kwa uwepo wa fursa kama hizi inakuwa rahisi kwetu kupata mbinu nyingine ya kujiongezea kipato,” anasema Pongwa.
Thamani na ubora wa ngozi
Meneja Uzalishaji wa KLICL, Edward, anasema kiwanda hicho kimekuwa kikikusanya ngozi kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Moshi, Arusha, Babati, Dodoma, Dar es Salaam, Morogoro na baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji na aina ya bidhaa zilizoagizwa na wateja.
Anasema mfumo wa ukusanyaji wa malighafi unahusisha mawakala pamoja na magari ya kampuni, ambayo hutumika kusafirisha ngozi kutoka maeneo mbalimbali kwenda kiwandani. “Tunataka mfugaji ajue kuwa anapofuga mnyama, si nyama pekee inayoweza kumpatia kipato, bali hata ngozi ina thamani na inaweza kuwa chanzo kingine cha mapato,” anasema.
Edward anaongeza kuwa KLICL hununua kilo moja ya ngozi ya ng’ombe kati ya Sh 800 na Sh 1,000, huku kipande kimoja cha ngozi ya mbuzi kikinunuliwa kati ya Sh 2,500 na Sh 3,000. Kuhusu ubora, meneja huyo anataja alama za chapa zinazopigwa kwenye mifugo na matundu yanayosababishwa na visu wakati wa uchunaji kuwa miongoni mwa sababu zinazopunguza ubora na thamani ya ngozi.
Kutokana na changamoto hiyo, KLICL imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Mifugo kutoa elimu kwa wafugaji na wachunaji kuhusu namna bora ya kutunza ubora wa ngozi. Elimu hiyo inahusisha matumizi ya hereni kutambua mifugo badala ya chapa, matumizi ya visu maalumu wakati wa kuchuna na upakaji wa chumvi kwenye ngozi mara baada ya kuchunwa ili kuzuia kuoza kabla ya kusafirishwa.
Mkoani Geita mchinjaji wa mifugo, Mashaka Innocent anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiuza ngozi kwa mawakala wanaonunua kwa bei ya kati ya Sh 400 na Sh 500 kwa kilo moja. Baadhi ya mawakala hao huingia makubaliano ya muda mrefu na wachinjaji ili kuhakikisha wanapata ngozi kwa ajili ya biashara zao.
Katika makubaliano hayo, anasema mawakala husika hutoa malipo ya awali yanayoweza kufikia Sh milioni tatu, huku kiasi hicho kikielezwa kufikia hadi Sh milioni 10 kwa wachinjaji wenye uwezo wa kuchinja ng’ombe sita kwa siku.
“Mpango huu ni mzuri, kwani umetusaidia kwa kiasi kikubwa kunyanyua mitaji yetu. Takriban miaka 10 sasa, ngozi zimekuwa zikienda kwa mawakala ambao hutuambia wanazipeleka katika kiwanda cha Kilimanjaro,” anasema.
Kauli hiyo inaashiria kuwa mawakala wanaofanya biashara na wachinjaji wa Geita ndiyo hupelekea malighafi hizo kwenye kiwanda cha KLICL licha ya tofauti kubwa ya bei. Pamoja na manufaa ya kupata soko la uhakika na mitaji kupitia malipo ya awali, Innocent anasema mfumo huo una changamoto, hasa katika bei wanazolipwa.
Anabainisha kuwa wachinjaji wengi hawana taarifa kuhusu masoko mengine ya ngozi wala uwezo wa kutafuta wanunuzi wa moja kwa moja, hali inayowafanya kutegemea mawakala wachache na kukubali bei wanazowapatia. “Changamoto ni kwamba bei bado si rafiki. Wananufaika wao, na sisi hatuyajui masoko mengine. Kwa hiyo tunakubali wanachotupa kwa sababu tunajua hatuna mitaji mikubwa,” anasema.

Kwa mtazamo wake, suluhisho ni kupanua wigo wa wanunuzi ili kuongeza ushindani na kuwapa wachinjaji nafasi ya kupata bei yenye tija zaidi na kwamba uwepo wa wanunuzi wengi, ikiwemo uwezekano wa viwanda kununua ngozi moja kwa moja kutoka kwa wachinjaji au kuongeza bei inayolipwa, unaweza kuboresha mapato yao na kuimarisha shughuli za uchinjaji.
“Sisi hatujawahi kutupa ngozi. Mteja wetu anatusaidia kuendesha biashara. Tukipata wateja zaidi wenye bei kubwa au kiwanda kikafikiria kutuongezea bei, itakuwa faraja kubwa sana kwetu,” anasema Innocent.
Ngozi kama lulu
Kaimu Mkurugenzi wa KLICL, Aligawesa, anasema kiwanda hicho sasa kinatumia mfumo wa uzalishaji kwa mikataba, unaowawezesha wafanyabiashara kuwasilisha miundo na mahitaji yao ili kutengeneza viatu na bidhaa nyingine za ngozi kwa chapa zao, bila kulazimika kuwa na viwanda vyao.
Anasema mfumo huo ni sehemu ya upanuzi wa shughuli za kiwanda, ambacho awali kilipangwa kuzalisha viatu vya majeshi pekee, lakini sasa kinazalisha pia viatu vya kiraia, soli, malapa na bidhaa nyingine za ngozi.
“Ushindani upo ila sisi tunajikita sana kwenye ubora na uimara. Ukiangalia vitu vinavyotoka nje kama mtoto wa shule atavaa miezi mitatu na anahitaji kwenda kubadilsiha, lakini sisi niwahakikishie mtoto atavaa zaidi ya mwaka,” anasema Aligawesa na kuongeza kuwa wanaomba Serikali kuendelea kukitangaza kiwanda hicho na vingine vya ndani.
Aligawesa anasema mbali na kuhudumia soko la ndani, kiwanda kimekuwa kikipokea oda kutoka nje ya nchi hasa barani Asia, huku baadhi ya wanunuzi wa kimataifa wakionesha nia ya kununua ngozi zilizochakatwa. “Tunapopokea oda ya bidhaa, tunazalisha kwa asilimia 100 ya mahitaji ya mteja. Kwa sasa tumeanza kuona wateja wengi kutoka nje ya nchi wanaokuja kuchukua ngozi,” anasema.
Taarifa za kisekta zinaonesha kuwa mahitaji ya ndani ya viatu yanafikia jozi milioni 46.8 kwa mwaka, huku nchi za Afrika Mashariki zikiagiza bidhaa za ngozi na viatu zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 566 kila mwaka.
Kwa upande mwingine, ushirikiano kati ya KLICL na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), uliosainiwa Juni 27, 2026 kwa lengo la kuimarisha ujuzi wa wataalamu, mafunzo kwa vitendo na utafiti katika teknolojia ya ngozi, unaweza kusaidia kupunguza pengo la ujuzi na kuongeza tija katika uzalishaji.



