RIO, Brazil
KUTOKA kuwa mmoja ya wachezaji watukutu barani Ulaya, Dani Alves ameamua kubadili aina ya maisha na sasa ni mchungaji aliyeshiba imani ya Dini ya Ukiristo akizunguka maeneo mbalimbali kuhubiri neno la Mungu.
Hivi karibuni, alikuwa nchini Argentina kuhubiri, ambako alifanya hivyo katika miji mikubwa miwili ya Formosa na Salta.
Hata hivyo, Alves aliyewahi kucheza Barcelona na Juventus, aliamua kugeukia upande huo wa maisha baada tu ya kutoka gerezani Machi 25, 2024.
Alikamatwa mwaka Januari 20, 2023, na kufunguliwa mashitaka ya udhalilishaji wa kingono dhidi ya mwanamke mmoja katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona.
Baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 23, ilimuhukumu kifungo cha miaka minne na miezi sita gerezani.
Alisota jela kwa miezi 14, kisha kuachiwa na tangu hapo akageuka kuwa ‘Malaika’ na kuanza kuwa muhubiri wa neno la Mungu.
“Unapaswa kuwa na imani ya Mungu. Mimi ni shuhuda wa hilo. Nimeunga urafiki na Mungu,” alisema mkongwe huyo wa kandanda.
Kwa sasa, Alves ni baba wa watoto watatu, ingawa mmoja wa kiume aliyezaliwa mwaka 2025 ndiye pekee aliyenaye kwenye ndoa yake na mkewe wa sasa, Joana Sanz, ambaye alifunga naye ndoa mwaka 2017.
Watoto wake wawili waliobaki, Daniel Jr. na Victoria, aliwapata katika ndoa yake ya kwanza na mrembo Dinorah Santana.


