Na mwandishi wetu, Gazetini- SHINYANGA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limewazawadia tokeni za umeme zenye thamani ya Sh 20,000 kila mmoja wazazi 27 waliojifungua katika Kituo cha Afya Kambarage mkoani Shinyanga, ikiwa ni ishara ya upendo na kushirikiana na jamii katika kuadhimisha miaka 95 ya shirika hilo.
Zawadi hiyo iliyotolewa Novemba 26, 2026, inalenga kuwasaidia wazazi hao kupata huduma ya umeme majumbani mwao na kuwapokea watoto wao katika mazingira yenye nishati ya umeme.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Emma Nyaki, amesema shirika hilo limetoa jumla ya Sh 540,000 kwa ajili ya kununua tokeni zitakazogawiwa kwa wazazi hao.
“Katika siku ya leo tumetoa tokeni za Sh 540,000 kwa wazazi 27 waliojifungua. Kila mzazi atapewa tokeni za Sh 20,000 ili kwenda kuwaangazia watoto hawa katika nyumba zao,” amesema Nyaki.
Mmoja wa wazazi walionufaika na zawadi hiyo, Jadida Hashimu, ameishukuru Tanesco kwa kuwapatia tokeni hizo, akisema pia wanathamini huduma ya umeme wanayoipata kutoka kwa shirika hilo.
“Naishukuru Tanesco kwa zawadi hii ya tokeni. Pia tunashukuru kwa huduma zao nzuri za kila siku, hatupati shida ya umeme,” amesema.
Kwa upande wake, Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kambarage, Paulina Kitambi, amelishukuru shirika hilo kwa kuonesha upendo kwa wazazi na watoto hao, akisema wamefurahishwa pia na chakula walichoandaliwa.
“Ninamshukuru Mungu kwa wazazi hawa 27 kujifungua salama. Pia niwashukuru TANESCO kwa kuonesha upendo kwa watoto hawa kupitia zawadi ya tokeni pamoja na kutuletea chakula. Tumefurahi sana, tunaomba jambo hili lisiishie leo bali liwe endelevu,” amesema Kitambi.
Katika hatua nyingine, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Hadija Mbaruku, amewataka wateja kuzingatia taratibu sahihi wanapotumia mifumo ya kujiunga na huduma za shirika hilo ili kurahisisha mawasiliano na upatikanaji wa huduma.
Amesema baadhi ya wateja wanapohitaji msaada wa kujiunga na huduma hutumia namba za simu za watu wanaowasaidia badala ya kuweka namba zao wenyewe, hali inayosababisha changamoto katika mawasiliano kati ya TANESCO na mteja husika.
“Kumekuwa na changamoto kwa wateja wetu kutokuwa na elimu ya kutumia mfumo wa kujiunga. Unakuta wanatafuta watu wa kuwasaidia, lakini hawaweki namba ya mteja husika; wanaweka namba zao. Inakuwa vigumu kuwasiliana na mteja husika kwa sababu watu hao wanasaidia wateja wengi,” amesema Mhandisi Mbaruku.



