26.6 C
New York

Vyakula hivi kiboko ya ugonjwa wa kiharusi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WATU takribani 795,000 hupata kiharusi (kupooza) kila mwaka nchini Marekani, huku wataalamu wakionya juu ya mtindo wa maisha, pia wakishauri aina ya vyakula vya kuzingatia ili kuepukana na maradhi hayo.

Ni vyakula vinavyopunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu, kiwango kikubwa cha mafuta na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, ambavyo ndivyo vichocheo vya kiarusi.

Hiyo ni kwa mujibu wa Cheng-Han Chen, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya moyo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya MemorialCare Saddleback nchini Marekani.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa tiba-lishe kutoka Chuo Kikuu cha Ohio, Kristine Dilley, anataja vyakula sahihi katika kukabiliana na ugonjwa wa kupooza, akianza na mboga za majani.

Kwamba mboga hizo zina madini ya nitrate, ambayo mwili huyabadili na kuwa nitric oxide inayosaidia mtiririko mzuri wa damu kwenye mishipa.

Katika utafiti mwingine wa mwaka 2021 uliochapishwa katika jarida la European Journal of Epidemiology, ilibainika kuwa mboga za majani, ikiwamo spinanchi, inapunguza ugonjwa wa kupooza kwa asilimia 17.

“Pia, kuna matunda, nafaka, maharage na hata samaki,” anasema Dilley na kusisitiza kuwa aina hiyo ya vyakula pia hushusha kiwango cha mafuta, hivyo kupunguza uzito wa mwili.

Aidha, mtaalamu wa tiba-lishe kutoka Taasisi ya Medical Nutrition Therapy, Scott Keatley, anaongeza kuwa vyakula hivyo zinaweza pia kupunguza shinikizo la damu na wakati huo huo kurahisisha utendaji-kazi wa mishipa ya damu.

Hata hivyo, Dkt. Chen anasisitiza juu ya umuhimu wa mpangilio sahihi (balanced diet) ili kuhakikisha kila aina ya chakula kinapatikana katika uwiano unaotakiwa.

Related articles

Recent articles