26.6 C
New York

Usajili unaoakisi uchumi wa klabu au mfuko wa tajiri?

Published:

Na Hassan Mwasha

NIMEFUATILIA ubize wa vigogo wa soka la Tanzania, Yanga na Simba, katika soko la usajili wa dirisha kubwa kuelekea msimu mpya wa 2026-27.

Kufikia hatua hii, hakuna aliyekubali kubaki nyuma. Ni mwendo wa kushusha ‘vyuma’ na kutambiana huko mitandaoni na hata kwenye vijiwe vya soka.

Naweza kusema usajili wa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Peter Shalulile, ndiyo ulioitikisa zaidi kwa upande wa Yanga.

Kwa Simba, ni ujio wa ‘fundi’ mwenzake kutoka Afrika Kusini, Kabelo Makgalwa, ambaye ni mmoja ya wachezaji wanaozungumziwa zaidi katika soka la nchi hiyo.

Aidha, usajili wa wachezaji daraja la juu kama Shalulile na Makgalwa unaakisi mambo makubwa matatu juu ya klabu za Yanga na Simba.

Mosi, ni wazi zimeamua kushindana kimataifa. Ni usajili unaoonesha kuwa zimedhamiria kufanya vizuri katika michuano ya nje, badala ya kushindania ukubwa ni Ligi, FA, Kombe la Muungano na Kombe la Mapinduzi.

Kuona Yanga ‘inavunja kibubu’ kwa ajili ya Shalulile inakupa picha kwamba sasa haijipangi tena kushindana na Simba, bali inahamishia vita kwa klabu za daraja la Mamelodi Sundowns.

Iko hivyo pia kwa Simba. Haimuhitaji Makgalwa ili kuzifunga JKT Tanzania, Mbeya City, Dodoma Jiji na timu zingine za daraja la kati. Uwekezaji uliofanywa kwa Makgalwa unailenga moja kwa moja michuano ya nje, hasa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pili, zimehamisha mwelekeo wa usajili. Tofauti na miaka mingi iliyopita, sasa Yanga na Simba zimeanza kujenga himaya yake katika soka la Afrika Kusini. Makocha wa timu zote mbili wanatoka ‘Sauzi’ na hata usajili wa wachezaji unawarudisha huko.

Unaweza kutabiri kuwa haitochukua muda mrefu kuiona Ligi Kuu Bara ikiwa imemezwa na wachezaji kutoka huko, kama ilivyowahi kutokea kwa Wacongo katika miaka ya hivi karibuni.

Tatu, tujiulize; usajili wa aina hii unaakisi ukuaji wa uchumi wa klabu za Simba na Yanga au ni uwezo wa kifedha wa mabosi/viongozi?

Ikiwa ni usajili unaoakisi ukuaji wa klabu, ni jambo zuri na la kujivunia kwa mashabiki na wanachama. Kwamba sasa Yanga na Simba hazitegemei mtu au kikundi cha watu fulani.

Kinyume chake, ikiwa ni mifuko ya mabosi ndiyo inayowasajili akina Makgalwa, basi bado changamoto ni kubwa. Bado zimebaki kuwa ni klabu zinazotegemea hisani si kujiendesha kwa uchumi wake.

Licha ya walio wengi kupumbazwa na matokeo ya uwanjani, moja ya majukumu nyeti waliyonayo viongozi wa Yanga na Simba ni kuzifanya klabu hizo ziweze kujiendesha.

Je, tuseme wamefanikiwa na sasa Yanga na Simba zina msuli wa kiuchumi wa kusajili wachezaji bora na kuajiri makocha wa daraja la juu kutoka Afrika Kusini?

Related articles

Recent articles