Na Malima Lubasha, Gazetini
MKUU wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Angelina Lubela, amezindua Jukwaa la Vijana (Youth Platform) ikiwa ni hatua ya kuimarisha ushiriki wa vijana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Lubela alitoa wito huo wakati akizindua jukwaa hilo jana katika Ukumbi wa Chuo cha Ukunga na Uuguzi cha Kisare, wilayani Serengeti. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa maendeleo.
Viongozi wengine walioshiriki uzinduzi huo ni Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati; Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Makuruma; pamoja na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Nyansaho Foundation, Benki ya Azania, TAKUKURU na Jeshi la Polisi.
Akizindua jukwaa hilo, Lubela aliwahimiza vijana kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ili kujikwamua kiuchumi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Pia aliwataka vijana kutumia fursa zilizopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali zitakazowaongezea kipato.
Aidha, aliwahimiza kuendelea kulinda amani na mshikamano, akisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira mazuri yanayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
“Tunayo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye wanyamapori wengi. Nawahimiza muanzishe vikundi na, ikiwezekana, muanze kuuza mboga mboga na bidhaa nyingine ili mnufaike na fursa zilizopo katika hifadhi hiyo,” amesema Lubela.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, aliwataka vijana kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara ili kubadilishana mawazo, kujifunza uzoefu na kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali za maendeleo.
“Vijana mnapaswa kuwa mstari wa mbele kutumia fursa zilizopo na zinazojitokeza, na kuepuka kukata tamaa,” amesema Surati.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Makuruma, aliwahimiza vijana kuwa na nidhamu, uadilifu na uaminifu, akisema maadili ndiyo msingi wa kujenga taifa lenye vijana wenye uwezo wa kuleta mabadiliko na maendeleo endelevu.


