20.6 C
New York

Beckham na mitego yake ya pesa inayompa maisha ya kibosi

Published:

LONDON, Uingereza

MEI, 2026, Gazeti la Sunday Times lilimtaja David Beckham kuwa ndiye mwanamichezo pekee wa Uingereza aliyefikia hadhi ya kuitwa bilionea.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari hicho, Beckham na Victoria wana utajiri wa Dola bilioni 1.58 na kwa sasa wanashika nafasi ya 141 katika orodha ya matajiri wa Uingereza.

Sehemu ya fedha hizo zilipatikana kupitia mishahara, posho na dili za matangazo akiwa mchezaji wa klabu za Manchester United, Real Madrid, LA Galaxy, AC Milan, na PSG.

Kama itakumbukwa, mwaka 2003, Jarida la France Football, waandaaji wa tuzo ya Ballon d’Or, lilimtaja kuwa ndiye mwanasoka anayelipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.

Hata hivyo, alipojiunga na LA Galaxy ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS) alitajwa kuvuna fedha nyingi zaidi.

Licha ya kwamba mshahara wake ilipungua kwa asilimia 70, ikilinganishwa na alipokuwa akipewa Madrid, posho na dili za matangazo ziliongezeka mara dufu akiwa MLS.

Katika ripoti yake, Sunday Times imedai kuwa Beckham alivuna takribani Dola milioni 225 akiwa na klabu hiyo.

Pia, ni katika mkataba ambao ulikuwa na kipengele kinachomruhusu kuwa sehemu ya wamiliki wa LA Galaxy.

Hivyo, licha ya kuwa mchezaji, pia Beckham alikuwa akipewa sehemu ya mapato ya klabu, achilia mbali mshahara na posho.

Kwa ujumla, Beckham alijikusanyia Dola milioni 800 katika kipindi chote cha maisha yake ya soka, kwa mujibu wa Gazeti la Mirror.

Alipostaafu mwaka 2013, nahodha huyo wa zamani wa timu ya soka ya Taifa ya England alinunua hisa katika klabu nyingine ya MLS, Inter Miami.

Inter Miami iliyoanzishwa mwaka 2018, kwa sasa inatajwa kuwa ndiyo klabu tajiri zaidi MLS (Dola bilioni 1.35).

Kwa upande wa dili za matangazo, Beckham (51), anafanya kazi na kampuni nyingi zinazomtumia kutangaza bidhaa zao. Baadhi yao ni H&M, Armani, Adidas, Breitling, Gillette, PepsiCo, na Maserati.

Miongoni mwa dili zinazosimamiwa na kampuni hiyo ni mkataba wake mnono na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas, ambao una thamani ya Dola milioni 160.

Mwaka 2014, alianzisha kampuni yake binafsi, DB Ventures, ambayo jukumu iliyonayo ni kusimamia dili anazopata.

Mwaka 2022, kampuni hiyo ilimuingizia zaidi ya Dola milioni 230 baada ya kuuza sehemu ya hisa zake.

Kipindi hicho pia, Beckham alisaini mkataba wenye thamani ya Dola milioni 166 na Serikali ya Qatar ili awe balozi wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini humo.

Itakumbukwa, mkataba huo ulimpa wakati mgumu mbele ya wanaharakati wa mapenzi ya jinsia moja, ambao waliona ameungana na Taifa lisilounga mkono vitendo hivyo.

Mwaka 2025, Mfalme wa Uingereza, Charles III, alimtunuku Beckham jina la ‘Sir’, ambalo hupewa watu wachache nchini humo kutokana na mchango wao kwenye jamii.

Kocha wake wa zamani wa Man United, Alex Ferguson, naye aliwahi kupewa heshima hiyo.

Beckham na Victoria walikutana katika miaka ya 1990, wakati huo bibiye akiwa memba wa Kundi la muziki wa Pop la ‘The Spice Girls’.

Tangu alipouweka kando muziki, Victoria amekuwa na mafanikio makubwa kwenye tasnia ya mitindo.

Wakati Beckham akiwa wa kwanza Uingereza, Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji wa kwanza (anayeendelea kucheza) kufikia hadhi ya kuitwa bilionea.

Nyota huyo wa timu ya soka ya Taifa ya Ureno, anavuna Dola milioni 180 kwa mwaka katika klabu yake ya Al Nassr ya nchini Saudi Arabia.

Related articles

Recent articles