WASHINGTON, Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema ameridhishwa na mwenendo wa mazungumzo ya maelewano kati ya Marekani na Iran, akidai kuwa Tehran inaonesha ushirikiano mkubwa katika hatua za sasa za majadiliano, huku akionya kuwa Washington iko tayari kuchukua hatua nyingine endapo makubaliano hayatatekelezwa kama inavyotaka.
Trump ametoa kauli hiyo katika taarifa yake ya hivi karibuni kwa waandishi wa habari, akieleza kuwa licha ya mvutano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili, kwa sasa Iran inaonekana kukubali masharti mengi yanayowekwa mezani na Marekani.
“Nani angefikiria hili lingetokea? Huu ni wakati wa vita na Iran ina tabia nzuri sana. Wanakubali kila kitu ninachouliza na wanapaswa kufanya. Vinginevyo, tutarudi tu na kufanya kile kinachohitajika,” alisema Trump.
Kauli hiyo imeibua tafsiri mpya kuhusu mwelekeo wa uhusiano wa Washington na Tehran, hasa wakati ambapo dunia imeendelea kufuatilia kwa karibu hatua za kidiplomasia zinazolenga kupunguza mvutano wa kisiasa na kijeshi kati ya pande hizo mbili.
Trump pia aligusia mwenendo wa soko la mafuta duniani, akisema hali ya sasa ya mazungumzo inakwenda sambamba na mabadiliko ya bei ya mafuta ambayo kwa sasa inakaribia dola 70 kwa pipa, ishara kwamba masoko yanaendelea kutathmini kwa karibu hatma ya mzozo huo.
Kauli ya rais huyo wa Marekani inakuja siku chache baada ya timu za mazungumzo kutoka Marekani na Iran kukutana nchini Uswizi katika juhudi za kutafuta mwafaka wa kidiplomasia. Taarifa zinaeleza kuwa mkutano huo ulifanikishwa kwa usuluhishi wa Pakistan, katika kile kinachoonekana kuwa sehemu ya jitihada za kimataifa za kuzuia kuongezeka kwa mzozo huo.
Hata hivyo, licha ya hatua hiyo kuonekana kufungua njia ya mazungumzo, hali bado inaendelea kuwa ya sintofahamu kufuatia maafisa kutoka nchi zote mbili kutoa kauli kali na wakati mwingine zinazokinzana kuhusu mustakabali wa mazungumzo hayo.
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaona kauli ya Trump kama sehemu ya mkakati wa kuonesha msimamo wa Marekani kuwa bado ina nguvu ya kushinikiza makubaliano, huku ikiweka wazi kuwa diplomasia pekee haitatosha iwapo Iran haitafuata masharti yanayowekwa.
Marekani na Iran zimekuwa katika mvutano wa muda mrefu unaohusisha masuala ya nyuklia, usalama wa Mashariki ya Kati, vikwazo vya kiuchumi na ushawishi wa kisiasa katika eneo hilo. Hivyo, kila hatua ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili inaendelea kuangaliwa kwa uzito mkubwa na jumuiya ya kimataifa kutokana na athari zake kwa usalama wa dunia na uchumi wa kimataifa.


