22 C
New York

Unajua kwa nini huajiriwi licha ya ‘interview’ nyingi?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

UNAJIULIZA kwanini hujapigiwa simu ya kuitwa kazini licha ya kuhisi ulifanya vizuri Siku ya usahili (interview)? Tulia.

Huenda tatizo si uwezo wako wa kufiti katika nafasi uliyoomba. Unaweza kuwa ni mtaalamu mzuri tu wa IT au Mauzo na Masoko, lakini ni mambo madogo tu yalikuangusha katika usahili.

MWONEKANO

Hili ni eneo linalochukuliwa poa lakini lina nafasi yake katika kuwashawihi waajiri. Hapa hauzungumziwi uzuri wa sura au umbo, bali utanashati wako mbele ya macho ya mwajiri.

Achana na kukuongezea hali ya kujiamini, wataalamu wa saikokojia wanaeleza kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya mwonekano mzuri na kiwango cha kukubalika, kuheshimika na kuaminika.

Nenda kwenye usahili wa kazi ukiwa umevaa na kunukia vizuri. Epuka mavazi yasiyo na staha, pia yenye kukunyima uhuru wa namna ya kukaa (sketi fupi kwa akina dada).

Ni vizuri pia kuchagua mavazi yanayoendana na kazi husika (siyo sare) kwani itamfanya mwajiri kukuona katika sura ya ‘mfanyakazi wake’ hata kabla ya kukuliza swali la kwanza.

WEWE NI NANI?

Linaweza kuonekana ni swali rahisi na lisilohitaji hata dakika tano kulijibu, lakini ni moja kati ya yale yanayokwamisha wengi wanapokuwa kwenye usahili wa kazi.

Unapoambiwa ujieleze, au ‘Tell us about yourself’, kama inavyotamkwa kwa Kiingereza, hutakiwi kuzungumzia maisha binafsi (umri, idadi ya watoto, kabila, n.k.).

Na badala yake, mwajiri wako mpya kwenye chumba cha usahili anataka kujua elimu na safari yako ya kitaaluma, hasa katika nafasi uliyoomba.

Katika historia ya elimu, wengi hujikuta wanajichanganya kwa kutaka kuanza na shule ya msingi, sekondari na elimu ya juu, kote huko wakilazimisha kutaja na miaka.

Hakuna anayehitaji yote hayo. Badala ya kote huko, unaweza kusema tu una Astashahada (Certificate), Stashahada (Diploma) au Shahada (Degree)  ya taaluma fulani, kisha kazi ulizofanya tangu ulipohitimu ngazi hiyo ya elimu.

Mwisho, tofauti yako na wengine itakuja pale utakapohitimisha kwa kugusia sababu ya kuomba kazi, ukisema elimu na uzoefu uliotaja vinaendana na nafasi iliyotangazwa.

UBORA, UDHAIFU WAKO

‘Wha is your strength? (Ni upi ubora wako?). Jikite katika masuala ya kawaida (uwezo wa kuwasiliana, kushirikiana na wenzako, kutekeleza majukumu pasi na kusimamiwa, n.k), ambayo kimsingi yataleta tija katika ustawi wa kampuni.

Kwa kumtambua kuwa hakuna binadamu aliyekamilika, hata waajiri wenyewe, epuka kujiona malaika pindi utakapoulizwa kuhusu uhalifu wako (weakness).

Hata hivyo, kuwa makini. Jikite katika madhaifu yasiyoathiri moja kwa moja utendaji katika nafasi ya kazi unayoomba. Mathalan, kusema ni ‘mlevi’ wa usingizi haifai katika usahili wa kazi ya ulinzi, siyo?

Madhaifu yanayokubalika ni kufanya kazi kupitiliza, hivyo kukosa muda wa kupumzika, aibu ya kuzungumza kwenye hadhara, kujikosoa hata pale unapokuwa umekosea jambo dogo, n.k.

KWANINI TUKUAJIRI, VIPI MSHAHARA?

Katika swali la ‘Why should we hire you?’, wengi huelezea sifa walizonazo kitaalamu. Siyo mbaya. Ndicho mwajiri anachotaka kusikia.

Hata hivyo, tofauti yako na wengine wanaotaka kazi hiyo, ni endapo utamuonesha mwajiri namna taaluma na uzoefu wako vinavyooana na nafasi iliyotangazwa.

Mathalan, kama anahitaji mtu wa Mauzo, basi uwezo wako wa kuwasiliana, uwezo wa kutengeneza matangazo, na kuendesha kurasa za mitandao ya kijamii vitaisadia nafasi hiyo ndani ya kampuni.

Kuhusu mshahara, haishahuriwi kutaja kiasi, na badala yake msisitizo wako uwe ni kupata ajira ya kukusaidia kukua zaidi kitaaluma. Endapo utalazimishwa kutaja, basi kiwe

KWANINI UNAACHA KAZI YA SASA?

Ni swali la mtego na wengi hunasa kwa kujikita katika kuchambua madhaifu ya kampuni walizotoka au wanazofanya nazo kazi. Ni kosa.

Mwajiri wako mpya hataki kusikia kuhusu kuchelewa kwa mshahara, ugomvi kati yako na bosi, kampuni kufilisika, na porojo zingine zenye sura hiyo.

Na badala yake, anatarajia mtazamo chanya (positive attitude) kwa kueleza kiu yako ya kutafuta nafasi nyingine ya kukua zaidi kitaaluma baada ya kampuni yako ya awali kukufikisha hapo ulipo.

UNA SWALI?

Waajiri hupenda kukuuliza mwishoni mwa usahili. Isivyo bahati, wengi kati ya wanaoomba kazi hudhani kusema ‘hapana’ ni bora zaidi ili kutowakera waajiri.

Kinyume chake, kusema huna swali huwa na maana moja tu kwa mwajiri, hujiamini na huna unachokijua kuhusu kampuni yake.

Lakini, kuwa makini. Epuka kuuliza kuhusu mambo yasiyoonesha utayari wako wa kazi. Mathalan, kuuliza kuhusu tarehe za mshahara, likizo, n.k.

Aidha, moja ya maswali yanayopendekezwa na wataalamu wengi, unashauriwa kuuliza juu ya nini kampuni hufanya katika kuwaendeleza kitaalamu wafanyakazi wake.

Related articles

Recent articles