20.5 C
New York

Hofu iliyobaki baada ya Marekani, Iran kumaliza vita

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

RAIS wa Marekani, Donald Trump, ameitangazia dunia kumalizika kwa vita vyao na Iran vilivyodumu kwa siku zaidi ya 100 huko Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesema sherehe ya kufurahia na kujipongeza itafanyika Ijumaa ya wiki hii nchini Uswis.

Ikumbukwe, Pakistan ilikuwa msuluhishi mkuu wa vita hivyo vilivyoanza Februari 28, 2026, baada ya Marekani kushirikiana na Israel kuishambulia Iran.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Baraza la Usalama la Iran, makubaliano yamezitaka pande zote kusisitisha operesheni za kijeshi, ikiwamo nchini Lebanon, ambako wanajeshi wa Israel wameweka kambi wakishambuliana na Kundi la kigaidi la Hezbollah.

Hofu iliyopo ni kwamba Iran ni mshirika mkubwa wa Hezbollah na Lebanon kwa ujumla na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliweka wazi kuwa wanajeshi wake watabaki Kusini mwa nchi hiyo.

Kusisitiza zaidi, wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, aliweka wazi msimamo wao huo akisema:

“Mimi na Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, tumeweka wazi sera ya wanajeshi wetu kubaki kwenye kanda za usalama nchini Lebanon, Syria na Gaza.”

Katz alisisitiza kuwa hawana muda maalumu wanaoweza kusema wataondoka katika maeneo hayo kwani wako kwa ajili ya kuilinda raia wa Israel dhidi ya vikundi vya kigaidi katika nchi hizo.

Israel imekuwa ikisitiza kuwa kukaa kwao Kusini mwa Lebanon ni kwa ajili ya kudhibiti mipango ya Hezbollah inayolitumia eneo hilo kupanga na kutekeleza mashambulizi nchini kwao.

Sasa, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati, Iran haiwezi kukaa kimya na kuheshimu makubaliano yake na Marekani endapo itaendelea kuona mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.

Pia, ili Iran ibaki kwenye makubaliano ya kusitisha vita, kama ilivyokubaliana na Marekani, itataka Israel iondoshe vikosi vyake ya kijeshi nchini Lebanon.

Mtazamo huo ndiyo anaouona pia Gideon Levy, ambaye ni mwandishi wa habari wa Gazeti la Haaretz nchini Israel.

“Moja ya changamoto kubwa zilizopo (katika makubaliano yaliyofikiwa na Marekani na Israel) ni hali inayoendelea Lebanon.

“Ni kwa sababu Iran ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuihusisha Lebanon katika makubaliano yake na Marekani. Sasa, sioni yatakavyofanya kazi, maana bado wanajeshi wa Israel wako Lebanon,” anasema.

Kwa upande mwingine, makubaliano kati ya Marekani na Iran yanatafsiriwa kuwa ni pigo kubwa kwa Israel na Waziri Mkuu wake, Netanyahu.

Kwa miaka mingi, Netanyahu amekuwa akiiweka Iran kwenye malengo yake, akipania kuipa wakati mgumu, kama si kuisambaratisha kabisa.

Kinyume chake, Israel haionekani kama mshindani wa Iran na wala haikuwa na nafasi katika mazungumzo ya kusitisha vita.

Hata wakati Rais Trump anatangaza kufikia makubaliano na Iran, alisema Israel inapaswa kuishukuru Serikali ya Marekani kwa kumaliza tatizo hilo.

Mbaya zaidi, ripoti zinaeleza kuwa katika makubaliano na Marekani, Iran haijapewa sharti lolote juu ya uhusiano wake na Hezbollah, hivyo kuiendelea kuiweka kwenye wakati mgumu Israel inayopambana na kundi hilo.

Related articles

Recent articles