Na mwandishi wetu, Gazetini
WANANCHI wa Wilaya za Gairo, Mpwapwa, Kongwa, Chamwino na Kiteto wanatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika zaidi kufuatia kukamilika kwa miradi ya kuimarisha mfumo wa usambazaji wa umeme iliyotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 10.5.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station), ufungaji wa Transfoma ya Kudhibiti Umeme (Automatic Voltage Regulator-AVR) yenye uwezo wa MVA 20 pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Zuzu hadi Mbande yenye urefu wa kilomita 92.
Akizindua miradi hiyo Juni 16, 2026 katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi.
Alisema kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo, hitilafu zilizokuwa zinatokea katika eneo moja zilisababisha kukatika kwa umeme katika wilaya nyingine kutokana na utegemezi wa njia moja ya usambazaji wa umeme.
“Kituo hiki kimeimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika. Hapo awali changamoto zilikuwa kubwa, hususan wakati wa mvua ambapo hitilafu katika wilaya moja ziliathiri huduma katika wilaya nyingine. Leo tunashuhudia matokeo ya uwekezaji huu kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Ndejembi.

Alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini kwa lengo la kuendana na ongezeko la mahitaji ya wananchi na kasi ya maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, alisema utekelezaji wa miradi hiyo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za umeme na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema kwa muda mrefu wilaya hizo zilitegemea njia moja ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Dodoma Mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
“Awali kulikuwa na njia moja ya kusambaza umeme inayopita katika wilaya tano tofauti. Kuongezeka kwa mahitaji ya umeme pamoja na fursa za uwekezaji kulianza kuleta changamoto katika utoaji wa huduma. Tangu miradi hii ilipoanza kufanya kazi, changamoto zilizokuwa zikiathiri huduma zimepungua kwa zaidi ya asilimia 90,” amesema Twange.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, aliwataka wananchi na wawekezaji kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuanzisha viwanda, biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa eneo hilo.
Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuongeza fursa za uwekezaji, kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika Wilaya za Gairo, Mpwapwa, Kongwa, Chamwino na Kiteto.


