17.4 C
New York

Siri ugomvi wa Van Gaal, Di Maria wakiwa Old Trafford

Published:

MANCHESTER, Uingereza

ANGEL di Maria alitua Manchester United mwaka 2014 akitokea Real Madrid, usajili wake wa Pauni milioni 59.7 ukivunja rekodi katika soka la Uingereza.

Chanzo ni uhusiano mbaya na kocha wake, Van Gaal. Kwanini wawili hao walikuwa hawaivi chungu kimoja? Zipo sababu kubwa mbili.

TATIZO LILIANZIA HAPA

Mosi, ilielezwa kuwa Van Gaal hakupendekeza ujio wa Di Maria, bali mabosi wa Man United waliamua wenyewe. Hivyo, kwa upande wake, haukuwa usajili sahihi kwenye mipango yake.

Pili, Van Gaal ni kocha anayependelea wachezaji kufuata maelekezo yake ndani ya uwanja. Kwa mujibu wake, Di Maria alifeli katika kila jukumu alilopewa ndani ya uwanja.

Hatimaye, Van Gaal alianza kumsugulisha benchi, kabla ya Di Maria kugomea safari ya ‘pre-season’ nchini Marekani, akishinikiza kujiunga na PSG iliyokuwa imetuma ofa ya Pauni milioni 44.3.

DI MARIA ANASEMAJE?

Kwa upande wake, Di Maria anasema Van Gaal alikuwa na chuki binafsi tu. “Nilianza vizuri (maisha yake akiwa United) lakini ghafla tulianza kuwa na vikao vingi kuzungumzia makosa yangu ndani ya uwanja,” amesema.

“Hakuwahi kuzungumzia mazuri, kila wakati alionao makosa tu. Mwishowe, nilichoka. Kama yote yanatokea; hupewi nafasi ya kucheza, mambo hayaendi sawa, na huna uhusiano mzuri ndani ya klabu, inakuharibu sana. Nilichukia kuwa pale.”

Anaongeza kuwa licha ya kuvamiwa na majambazi akiwa PSG, bado alidumu na klabu hiyo miaka miwili baada ya kuondoka Man United kwa sababu maisha yalikuwa mazuri.

MKE NAYE AFUNGUKA

Mwaka 2022, mke wa Di Maria, Jorgelina Cardoso, naye aliponda maisha yao jijini Manchester, akisema yalikuwa ya hovyo, ikilinganishwa na walivyokuwa Madrid, Hispania.

“Mimi na Angel tulikuwa Madrid, katika moja ya klabu kubwa duniani. Vyakula vizuri, hali ya hewa nzuri, kila kitu kilikuwa kizuri,” alisema Jorgelina.

Jorgelina alifichua pia alivyojaribu kumshawishi Di Maria kukataa ofa ya Man United lakini mchezaji huyo alimwambia ilikuwa kubwa mno kwa masilahi yao.

DI MARIA YUKO WAPI SASA?

Baada ya kuzunguka kwa mafanikio makubwa katika soka la Ulaya, kwa sasa winga huyo yuko kwao, Argentina, ambako anaitumikia Rosario Central ya Ligi Kuu nchini humo.

Di Maria alijiunga na klabu hiyo Julai, 2025, akitokea Ligi Kuu ya Ureno alikokuwa akiitumikia klabu yake ya zamani ya Benfica.

Related articles

Recent articles