MERSEYSIDE, Uingereza
LIVERPOOL waliuanza msimu huu wa 2025-26 wakiwa na matarajio makubwa ya kufanya vizuri baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita.
Si tu waliingia msimu huu wakiwa mabingwa watetezi, bali pia walitumia Pauni milioni 450 kusajili nyota wapya 15 (kiangazi, 2025, na Januari, 2026) ili kuimarisha kikosi chao.
Hata hivyo, mambo hayakwenda kama walivyotarajia, na badala yake wamemaliza msimu huu wakiwa hawana taji lolote mkononi.
Katika Ligi, wamemaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo, waliishia robo fainali kwa upande wa FA, walikwamia raundi ya nne ya EFL Cup, na safari yao Ligi ya Mabingwa iliishia robo fainali.
Licha ya kufunga mabao 99, waliruhusu nyavu zao kutikiswa mara 76 kwenye michuano yote waliyoshiriki vijana hao wa kocha Arne Slot.
Licha ya Liverpool kutokuwa na mwenendo mzuri, straika raia wa Ufaransa, Hugo Ekitike, ndiye aliyeonekana kuwa shujaa wa kikosi, akifunga jumla ya mabao 16 katika michuano mbalimbali.
Mshambuliaji huyo alifunga mabao 11 kwenye Ligi, matatu ya Ligi ya Mabingwa, moja katika Kombe la FA, na moja kwa upande wa EFL Cup.
Isivyo bahati, Liverpool ilikosa huduma yake katika mechi za mwisho baada ya Ekitike kuumia Aprili, 2026, wakati timu hiyo ilipomenyana na matajiri wa Paris, PSG.
Hata hivyo, Dominik Szoboszlai anastahili kuwa Mchezaji Bora wa Liverpool kwa msimu wa 2025-26, ambapo ndiye aliyeongoza kwa kuhusika katika mabao mengi, akifunga 13 na kutoa ‘asisti’ 12.
Kwa upande mwingine, mambo hayakwenda kama yalivyotarajiwa kwa straika wa bei mbaya, Alexander Isak, ambaye Liverpool walimsajili kwa ada ya Pauni milioni 125 akitokea Newcastle United. Amemaliza msimu wa EPL akiwa na mabao matatu tu.


