20.9 C
New York

Mtazamo wangu kuhusu uteuzi wa Haji Manara kwa soka la Tanzania

Published:

Na Hassan Mwasha Gazetini

WIKI kadhaa zilizopita Ofisa habari wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Haji Manara, ameteuliwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, kuwa Msemaji wa timu zote za soka za taifa, ikiwamo Taifa Stars.

Mbali na Taifa Stars, Manara atakuwa Msemaji wa Serengeti Boys, Serengeti Girls, Twiga Stars na Ngorongoro Heroes, akiratibu mawasiliano katika timu hizo chini ya Baraza la Michezo nchini (BMT).

Kufuatia uteuzi huo, ni wazi kuwa Manara ‘Bughatti’ ni mtu sahihi na pia ni wakati sahihi kwake kupewa nafasi hiyo. Kwanini? Makala haya yanachambua.

Mosi, tunaweza kukubaliana kuwa Manara ni miongoni mwa viumbe wachache, kama siyo pekee, wenye ushawishi mkubwa katika medani ya michezo hapa nchini.

Inaweza kuwepo mifano mingi kuthibitisha hilo, ikiwamo idadi kubwa ya ushawishi wake mitandaoni, lakini kubwa zaidi ni historia yake ya kufanya kazi na klabu zote kubwa hapa nchini, Simba na Yanga.

Kwa kipindi chote cha uhai wa soka la Tanzania, Manara ndiye mtu pekee aliyeweza kufanya kazi Simba na Yanga katika nafasi ya uongozi.

Alikuwa Simba akiwa Ofisa Habari, kabla ya kuhamia Yanga na kushika nafasi hiyo hiyo. Haikuwahi kutokea kwa kiongozi mwingine kufanya hivyo tangu kuanzishwa kwa klabu hizo.

Ilivyo bahati kwake, licha ya kufanya kazi katika klabu hizo zenye ushindani mkali na wa kihistoria, Manara amebaki kuwa kipenzi cha mashabiki wa soka wa pande zote mbili (Simba na Yanga).

Ukiweka kando upekee wake huo, Manara, mtoto wa lejendari wa soka la Tanzania, Sunday Manara ‘Computer’, ana uzoefu wa miaka zaidi ya 20 kwenye nafasi aliyopewa na Makonda, hiyo ikitosha kuthibitisha kuwa ni mtu sahihi.

Pili, kwa miaka mingi, mashabiki wa soka hapa nchini wamekuwa na mwitikio mdogo linapokuja suala la timu za Taifa. Mahudhurio ya viwanjani yamekuwa hayaridhishi, si tu kwa Taifa Stars, bali pia kwa timu zingine za taifa.

Mara kadhaa mamlaka zimejaribu kuondosha viingilio lakini bado idadi ya mashabiki walioingia viwanjani imekuwa ndogo, ukilinganisha na Simba na Yanga zinapocheza hata mechi za kiraiki.

Uzuri wa Manara ni historia yake ya kushinda vita za aina hii. Alifaulu kwa kiasi kikubwa katika hilo akiwa na klabu zote mbili, hasa alipokuwa Simba.

Nguvu yake ya ushawishi iliongeza mashabiki viwanjani, hata pale timu hiyo ilipokuwa ikiandamwa na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha.

Hivyo, matarajio ni kwamba Manara ana uwezo wa kuzitumia njia hizo kurejesha mashabiki waliopotea katika mechi za Stars na timu zingine za taifa.

Pia, kuzifanya ziwe sehemu ya mijadala ya soka, kama zilivyo Simba na Yanga, tofauti na sasa.

Tatu, ni wakati sahihi. Tanzania ikiwa sehemu ya wenyeji watatu, itaziandaa fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) kwa kushirikiana na majirani zake wa Ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kenya na Uganda.

Si tu kujaza mashabiki, Manara ana ‘dunia’ yake ya ushawishi kwa wachezaji. Uwezo wake wa kuwajenga kisaikolojia, kama alivyofanya akiwa Simba na Yanga, unaweza kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa Stars katika michuano hiyo.

+255 744 187 871

Related articles

Recent articles