27.7 C
New York

Uadui unaozaliwa katikati ya urafiki wa Marekani, Israel

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

VYOMBO vya habari vya Marekani vimeripoti taarifa inayoashiria kuwapo kwa hali ya kutokuamiana kati ya Taifa hilo na Israel, ambao ni washirika wake wa miaka mingi.

Chanzo ndani ya Shirika la Usalama la Marekani (DIA) kilichonukuliwa na vyombo hivyo kimedai kuwa Marekani inaiona Israel kama mdukuaji hatari zaidi wa taarifa zake za kiusalama.

Kwa mtazamo wa wachambuzi wa siasa za ulimwengu, inaibua sura mpya ya uadui katikati ya urafiki wa nchi hizo, licha ya kukanushwa na pande zote mbili (DIA na Israel).

Aidha, wachambuzi wanaziona taarifa hizo kuwa ni mwendelezo wa utamaduni wa miaka mingi wa mataifa makubwa duniani kutokuaminiana katika masuala ya kiusalama.

Mwaka 2013, itakumbukwa kuwa aliyekuwa Kansela wa Ujerumani wakati huo, Angela Merkel, alihamaki baada ya taarifa za majasusi wa Marekani (NSA) kudukua simu yake ya mkononi.

Hata hivyo, ilikuja kudungulika kuwa Ujerumani kupitia Shirika lake la ujasusi la BND limekuwa na kawaida ya kudukua taarifa za washirika wake.

Mtaalamu wa masuala ya usalama wa Ujerumani, Erich Schmidt-Eenboom, anasema nchi nyingi duniani zimekuwa na kawaida ya kudukua taarifa za marafiki zao, hivyo hata kwa Israel na Marekani si jambo la kushangaza.

Pia, historia inaonesha kuwa Israel imeshawahi kudukua taarifa za Marekani, kama ilivyofanya mwaka 1987, ambapo ilimtumia mtaalamu wa jeshi la majini la marafiki zao hao, Jonathan Pollard, kupata taarifa.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Times, Pollard alikuwa akilipwa fedha nyingi na Israel kuvujisha kila taarifa muhimu ya usalama iliyoihusu Marekani.

Baada ya ‘msaliti’ huyo kubainika na kukiri, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani, ingawa Israel ilipaza sauti kumkingia kifua hadi alipoachiwa kwa masharti mwaka 2015.

Moja ya sharti likawa ni Pollard kwenda kuishi Israel mwaka 2020. Kitendo cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu, kumpokea uwanja wa ndege kilitafsiriwa kuwa ni dharau kwa Marekani.

Mwaka 2004, mchambuzi wa siasa katika Idara ya Ulinzi ya Marekani, Lawrence Franklin, naye aliingia kwenye mtego wa aina hiyo, akitajwa kuiuzia Israel taarifa nyeti za nchi hiyo.

Kwa upande wake, Marekani nayo imekwaa mara kadhaa kashfa ya kudukua taarifa za nchi zingine, zikiwamo Ujerumani (kama ilivyoelezwa awali) na Ufaransa.

Mwaka 2023, zilivuja nyaraka zilizofichua namna majasusi wa Marekani walivyonasa mazungumzo ya ndani ya viongozi wa Serikali ya Korea ya Kaskazini.

Taarifa za sasa, kwamba Israel inaidukua Marekani, zinakuja wakati viongozi wa nchi hizo, Netanyahu na Donald Trump, wakiwa kwenye hali ya kutokuelewana.

Wakati Trump akipambana kutafuta suluhu na Iran huko Mashariki ya Kati, hamuoni Netanyahu akifanya jitihada zozote kubwa za kumaliza vita walivyovianzisha pamoja dhidi ya Taifa hilo la Kiarabu.

Related articles

Recent articles