Na mwandishi wetu, Gazetini
FEBRUARI 19, 2025, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Palamaganda Kabudi, alisema Serikali imeamua kuutambua rasmi muziki wa Singeli kama alama ya Tanzania.
“Wizara na nchi imeamua tuchukue muziki mmoja na kuufanya alama ya Tanzania, hii haina maana kuwa muziki mwingine imewekwa kando ila tumeona imefika wakati tujitanabaishe kama taifa ili dunia ikisikia wimbo huo inajua ni Tanzania,” alisema.
Leo hii unaposoma makala haya, ni mwaka mmoja na miezi takribani mitano tangu Waziri Kabudi alipotoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari.
Je, muziki wa Singeli umepiga hatua gani kubwa tangu Februari 19, 2025, ili kuilinda hadhi kubwa iliopewa na Serikali ya Awamu ya Sita?
Tuanzie hapa; baada tu ya Serikali kuitambua Singeli kama nembo ya nchi, matarajio yalikuwa ni kuuona muziki huo ukichanua zaidi na wawekazaji wa biashara ya muziki wakihamia moja kwa moja kwenye muziki huo.
Wakati mwingine, zilikuwapo dhana kuwa huenda hata wasanii wakubwa wa aina zingine za muziki wakaondoka huko na kuhamia Singeli.
Isivyo bahati, hakuna lililotokea kati ya hayo mawili. Kwa ufupi, bado Singeli, kwa kiasi kikubwa, umebaki kuwa ni muziki ule ule.
“Ukiangalia hata kwenye promo ya nyimbo za Singeli au ‘branding’ za wasanii wake, bado ni za kawaida, tofauti na wenza wao Bongo Fleva,” anasema Suddy Mkawi, ambaye ni prodyuza wa muziki Kinondoni jijini es Salaam.
Suddy, maarufu kwa jina la ‘Double’, anaamini bado wasanii wa Singeli wanaishi kimtaani, ambako ndiko chimbumo la muziki huo, badala ya kubadilika ili kuendana na soko la kimataifa.
Wakati huo huo, baada ya kauli ile ya Waziri Kabudi, ungetarajia kuona wasanii wa Singeli wakitumia fursa hiyo kwa kufanya ‘kolabo’ nyingi na wasanii wa nje ili kuutanua muziki wao. Hilo pia halijatokea.
“Sasa hilo ni suala la menejimenti. Lazima wasanii wa Singeli wapunguze kuishi kwa mazoea. Wawe na timu zenye watu wenye weledi wa kuwasimamia, badala ya kuchukua washikaji tu,” anasema Pauline Kija ‘Drone’, mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam, ambaye ni msanii chipukizi wa Singeli.
Mbali na kutokuona kolabo hizo, pia ukame wa safari za nje, bado ni wasanii wachache wa Singeli wenye uwezo wa kufanya shoo zao wenyewe za ndani ya nchi, pasi na kutegemea uwepo wa wasanii wa aina zingine za muziki.
Kwamba kama anavyofanya Marioo, basi MCZO Morfan naye awe na uwezo wa kujaza mashabiki kwenye shoo yake mwenyewe Mlimani City.

Max Mzote, maarufu kwa jina la ‘MX’ ni mkazi wa Buguruni, Dar es Salaam, ambaye pia ni mchambuzi wa muziki wa kizazi kipya, anasema:
“Inaweza isiwe sahihi kwa asilimia 100 kuwaweka levo moja na Diamond Platinumz, lakini baada ya kauli ya Kabudi ungetegemea kuona wasanii wa Singeli wakianza kuonesha kile ilichokiona Serikali kutoka kwao.”
Mwisho, muziki wa Singeli bado unakua. Ni tofauti na R&B au Hip Hop, ambayo imekuwa kwenye soko la muziki wa kizazi kipya hapa nchini kwa miaka mingi.
Hivyo, bado wasanii wa Singeli wana muda wa kujifunza kutoka kwa wenzao hao na kubadilika ili kufikia matarajio ya Serikali – kuuona muziki huo ukiwa alama ya nchi.


