26.3 C
New York

Wakulima waiomba Serikali kuwaingiza kwenye mafunzo ya hifadhi ya jamii

Published:

Na Seif Takaza, Singida

WAKULIMA mkoani Singida wameiomba Serikali kuweka mfumo rasmi wa kuwaingiza kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ili waweze kunufaika na mafao ya uzeeni na kuwa na uhakika wa maisha bora baada ya kuacha shughuli za kilimo.

Wito huo umetolewa jana na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo (Amcos) wakati wa mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida uliofanyika mkoani humo.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Athumani Iddi kutoka Umoja Amcos ya Kata ya Mtoa, Tarafa ya Shelui Wilaya ya Iramba, alisema wakulima wanategemea mapato yatokanayo na mazao yao, hivyo ipo haja ya kuwaandalia mfumo rasmi wa akiba utakaowasaidia kumudu maisha yao wanapozeeka.

Iddi alipendekeza kuwepo kwa utaratibu wa kukata sehemu ya mapato yatokanayo na mauzo ya mazao kupitia vyama vya msingi na kuelekezwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya pensheni ya baadaye.

Alisema watumishi wa umma na baadhi ya wafanyakazi wa sekta binafsi hunufaika na mafao baada ya kustaafu kutokana na michango yao, hivyo wakulima nao wanapaswa kuwekewa mfumo rafiki wa hifadhi ya jamii utakaowapa kinga ya kiuchumi wanapoingia uzeeni.

Akijibu hoja hiyo, Afisa Ushirika wa Wilaya ya Manyoni, Christopher Lyamuganda, alisema utekelezaji wa pendekezo hilo unahitaji maandalizi ya sera na sheria zitakazojadiliwa na kupitishwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika rasmi.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Nuria Gulamali, alivielekeza vyama vya ushirika kutumia akaunti za benki katika shughuli zote za kifedha ili kuimarisha uwazi na kudhibiti ubadhirifu wa fedha za wakulima.

Pia alipiga marufuku vyama vya ushirika kupokea fedha taslimu kutoka kwa wanunuzi wa mazao na kusisitiza malipo yote yafanyike kupitia benki kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.

Aidha, alisema viongozi wa vyama hawapaswi kutumia simu binafsi kupokea fedha za vyama na kuwahimiza wakulima kufungua akaunti za benki ili kurahisisha malipo na kuongeza usalama wa fedha zao.

Kaulimbiu ya ushirika mwaka 2026 ni “Ushirika kwa Dunia Yenye Amani, Linda Ushirika, Chagua Uadilifu.”

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Singida, Daudi Ngayaula, aliwataka wakulima, viongozi na jamii kwa ujumla kudumisha amani na mshikamano ili kuwezesha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo bila hofu.

Alisema migogoro na kukosekana kwa amani vinaweza kudhoofisha juhudi za maendeleo na kuathiri mafanikio ya vyama vya ushirika pamoja na ustawi wa wakulima.

Related articles

Recent articles