Na wandishi wetu, Gazetini
Mpango huo umetajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Green Corridor Initiative unaolenga kuunganisha njia za kijani katika maeneo ya mijini ili kusaidia kupunguza joto, kusafisha hewa na kuboresha mazingira ya makazi.
Uzinduzi wa shughuli hiyo umefanyika sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Mazingira Duniani 2026, ambapo wananchi, viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa sekta binafsi walishiriki pia kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo.
Miti hiyo ilipandwa katika eneo lenye urefu wa kilomita tatu kutoka Uhasibu hadi makutano ya Oilcom.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alisema uhifadhi wa mazingira unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila mkazi wa wilaya hiyo.
“Iwe wewe ni mpangaji au mwenye nyumba, kama unaishi Temeke lazima uwe na miti mitano. Chagua mwenyewe kama ni miti ya matunda au ya kivuli,” alisema Mapunda.
Alisema upandaji miti ni njia mojawapo rahisi na yenye gharama nafuu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto zinazosababishwa na ongezeko la watu mijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Ever Green Landscaping, Amir Mpungwe, alisema tofauti ya mpango huo ni kwamba unalenga kuunda mistari endelevu ya miti badala ya upandaji wa miti katika maeneo madogo yaliyotawanyika.
“Tunataka kuona barabara kuu na maeneo ya umma yakigeuka kuwa njia za kijani zinazotoa kivuli, kupunguza joto na kuboresha ubora wa hewa kwa manufaa ya wakazi wote wa Dar es Salaam,” alisema Mpungwe.
Alisema Barabara ya Mandela ni mwanzo tu wa utekelezaji wa mpango huo, huku matarajio yakiwa ni kuupanua katika manispaa zote za Temeke, Ilala na Kinondoni.
Mpungwe aliwashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Bytrade, NatureRipe Kilimanjaro Limited na Mabwepande Compost Facility kwa kuunga mkono juhudi hizo za mazingira.
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka Juni 5, ikiwa ilianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1972 baada ya Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira ya Binadamu uliofanyika Stockholm, Sweden.


