LAGOS, Nigeria
MWANAMUZIKI wa Afrobeats nchini Nigeria, Ice Prince Zamani, amedai kuwa alitumia Naira milioni 340 (zaidi ya Sh mil. 630 za Tanzania) kununua bangi.
Akihojiwa kupitia kipindi cha televisheni cha ‘Black Box’, Ice Prince, ambaye anatamba na wimbo ‘Aboki’, amesema fedha hizo zilikwisha ndani ya miaka sita tu.
Pia, amesema zote zilikwenda kwa muuzaji mmoja kuanzia mwaka 2020 hadi 2026, achilia alizonunua kwa wengine katika mitaa ya Abuja, Jos, Ghana na London.
“Kuanzia mwaka 2020 hadi 2026, nilitumia Naira milioni 340 kwa ajili ya bangi tu,” amesisitiza staa huyo, ambaye kwa sasa ameachana na matumizi ya dawa hizo za kulevya.
Katika hatua nyingine, amewataka vijana kuachana na matumizi ya bangi, akisema si tu yana athari za kiafya, bali pia ni tatizo kiuchumi.


