12.9 C
New York

Wazazi wanauza watoto ili kumudu gharama za maisha

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA kila watu wanne nchini Afghanistan, watatu hawamudu mahitaji ya msingi, ambayo ni chakula, mavazi na makazi, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN).

Uhaba wa ajira ndiyo chanzo cha tatizo hilo na sasa vijana takribani milioni 4.7 wako hatarini kukumbwa na balaa la njaa endapo hali ya uhaba wa ajira itaendelea kuwa mbaya kwa kiwango hicho.

Aidha, wakazi wa Jimbo la Ghor ni wahanga wakubwa zaidi. Vijana na wanaume wa eneo hilo wako kwenye shimo la msongo wa mawazo kutokana na changamoto ya kukosa ajira.

Kwa upande mwingine, akina baba katika Jimbo la Ghor mjini Chaghcharan, Afghanistan, ndiyo wanaoumia zaidi kutokana na kukosa ajira za kuendesha maisha ya familia zao.

Juma Khan (45), mmoja ya wakazi wa eneo hilo, anasema kuliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa katika wiki sita za hivi karibuni, ni siku tatu pekee alizobahatika kupata kibarua.

Kwa siku tatu hizo, alivuna chini ya Dola 15. “Watoto wangu walilala njaa siku tatu mfululizo. Mke wangu alikuwa analia tu, kama ilivyokuwa kwa watoto. Nililazimika kwenda kwa jirani kuomba pesa ili ninunue unga. Nahofia watoto wangu watakufa njaa,” anasema Khan.

Kwa upande wake, Khwaja Ahmad anasimulia alivyopoteza mtoto wake wa kwanza kutokana na njaa. “Njaa inatutesa. Mtoto wangu wa kwanza alipoteza maisha. Nahitaji kazi ya kulisha familia. Lakini, tayari nimeshazee, hakuna anayetaka kuniajiri,” amesema.

Katika hatua nyingine, ugumu wa maisha umewasukuma baadhi ya akina baba kuwauza watoto wao kwa kuwaozesha au kazi za ndani ili kupata fedha za kuhudumia familia.

Abdul Rashid Azimi, baba wa watoto wanne, wakiwamo mapacha wa kike wenye umri wa miaka saba, ni miongoni mwa walioiona njia hiyo kama mkombozi. “Niko tayari kuwauza mabinti zangu. Mimi ni masikini, nina madeni na sina msaada,” amesema.

“Narudi nyumbani nikiwa nimekauka mdomo, nina njaa na kiu, nina msongo wa mawazo na nimechanganyikiwa. Watoto wangu wanakuja na kuniambia ‘Baba, tunaomba mkate’. Nitawapa nini na sina kazi?”

Abdul anasema yuko tayari kuwauza mabinti zake kwa wanaotoka kuwaoa au kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za ndani. “Nikiuza binti mmoja, naweza kulisha familia kwa walau miaka minne,” anasema.

Huku akimbusu binti yake mmoja na kumwaga machozi, Abdul anasema inamuumiza kuona analazimika kuwauza watoto wake ili kumudu gharama za maisha. “Kitu pekee tulichonacho hapa ni mkate na maji ya moto. Hatuna hata sukari,” anasema.

Watoto wa kiume wawili wa Abdul nao hawana kipato cha kutosha kuisaidia familia, licha ya kwamba ni wakubwa. Mmoja ni fundi viatu na mwingine anaokota takataka ili kujikimu.

Wakati huo huo, Saeed Ahmad ameiambia BBC kuwa ameuza binti yake mwenye umri wa miaka mitano aitwaye Shaiqa. Uamuzi huo ulikuja baada ya mtoto huyo kupata tatizo la kidole-tumbo na familia haikuwa na uwezo wa kuhudumia matibabu yake.

Shaiqa aliuzwa kwa Dola 3,200. “Sikuwa na pesa za kulipigia gharama za matibabu. Hivyo, nilimuuza binti yangu kwa ndugu,” amesema na kuongeza: “Kama ningekuwa na pesa, nisingechukua uamuzi huo.”

Ugumu wa maisha nchini Afghanistan umechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ya wahisani wakubwa wa kiuchumi, Marekani, kusitisha misaada. Pia, mataifa kama Uingereza yamepunguza michango yao.

Takwimu za UN zinaonesha kuwa misaada ya nje kwa Afghanistan imepungua kwa asilimia 70, ikilinganishwa na ile ya mwaka 2025.

Hali ya ukame iliyokumba nusu ya majimbo ya nchi hiyo nayo inatajwa kuchoche janga la njaa. “Hatuna msaada kabisa, siyo kutoka Serikalini wala asasi za kiraia,” anasema Abdul Malik.

Serikali ya Taliban iliyochukua madaraka mwaka 2021 inautupia lawama uongozi uliopita, ikisema iliruhusu Marekani kuharibu uchumi wa Afghanistan.

Hata hivyo, Taliban inatupiwa lawama kwa misimamo yake, hasa ukandamizaji wa haki za binadamu, ikitajwa kusababisha wahisani aidha kupunguza au kusitisha misaada kwa Taifa hilo la Kiarabu.

Related articles

Recent articles