21.9 C
New York

Waliondoka Simba, Yanga wakatwaa ubingwa wa CAF

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

MC Alger kutwaa taji la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wikiendi iliyopita, ambapo iliifunga Zamalek kwa penalti 8-7, ni stori kubwa katika maisha ya soka ya beki wa kati wa zamani wa Simba raia wa Cameroon, Che Malone.

Che Malone aliukosa ubingwa huo msimu uliopita (2024-25) akiwa na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, ambapo walipoteza fainali kwa kufungwa na vigogo wa soka la Morocco, RS Berkane.

“Nilizaliwa kuwa bingwa. Nilishindwa mara moja lakini si mara ya pili. Sisi ni mabingwa wa 2026,” amesema Che Malone kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Kwa upande mwingine, Che Malone anaingia kwenye orodha ya wachezaji wa kimataifa walionyakua taji la CAF baada ya kuondoka katika klabu za Simba na Yanga.

MBWANA SAMATTA

Mei, 2011, Samatta aliondoka Simba na kujiunga na TP Mazembe ya DRC. Miaka minne baadaye, mshambuliaji huyo alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na vigogo hao wa Lubumbashi.

Ikumbukwe, ni msimu ambao pia alikuwa mfungaji bora wa mashindano hayo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora anayecheza Afrika. Aliondoka TP Mazembe mwaka 2016 na kutua Genk ya Ubelgiji.

TUISILA KISINDA

Aliondoka Yanga Agosti, 2021 na mwaka mmoja tu baadaye alikuwa sehemu ya kikosi cha RS Bekane kilichonyakua ubingwa wa Kombe la  Afrika.

Ikiwa chini ya kocha wa sasa wa Azam, Florent Ibenge, RS Berkane iliifunga Orlando Pirates kwa penalti 5-4 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio mjini Uyo, Nigeria.

LUIS MIQUISSONE

Agosti, 2021, winga huyo wa kimataifa wa Malawi alitua Al Ahly kitokea Simba na miezi minne tu baadaye alitwaa ubingwa wa Super Cup akiwa na Wamisri hao.

Mchezo huo unaokutanisha mshindi wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho uliikutanisha Al Ahly na Raja Casablanca. Al Ahly walishinda kwa penalti 6-5 baada ya sare ya bao 1-1.

FISTON MAYELE

Julai, 2023, mshambuliaji huyo raia wa DRC alitua Pyramids ya Misri baada ya kiwango bora alichokionesha akiwa Yanga, ikiwamo kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika msimu wake wa pili, 2024-25, alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, tena akiibuka na tuzo ya mfungaji bora wa mashindano. Mwaka 2025, aliiongoza Pyramids kutwaa ubingwa wa CAF Super Cup.

Related articles

Recent articles