Na Hassan Mwasha, Gazetini
KUFIKIA hatua hii ya msimu wa Ligi Kuu Bara 2025-26, ambapo kila timu kati ya zile 16 imeshashuka dimbani mara 23 na kubakiza mechi saba, Simba ina rekodi yake ya kibabe.
Iko hivi; kwa sasa, Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo, ikizidiwa mbili na Yanga yenye 54, ndiyo timu pekee ambayo haijafungwa ugenini, licha ya kucheza mechi 12.
Katika mechi hizo, Simba ya kocha raia wa Afrika ya Kusini, Steve Barker, imeshinda mara saba na kutoa sare tano, imefunga mabao 18 na kuruhusu manne.
Kati ya pointi 52 walizonazo mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu, 26 walizivuna kupitia mechi zao za ugenini, idadi kubwa zaidi, ukilinganisha na timu zote msimu huu.
Yanga na Azam zinashika nafasi ya pili nyuma ya Wekundu wa Msimbazi baada ya kila moja kufungwa mechi moja kati ya 12 ilizocheza ugenini.


