GENEVA, Uswiz
Hofu imeendelea kuongezeka duniani kufuatia mlipuko wa virusi vya Hanta (Hantavirus) ulioripotiwa ndani ya meli ya kifahari ya kitalii ya MV Hondius, baada ya watu watatu kupoteza maisha na wengine kadhaa kuendelea kupata matibabu. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limewahakikishia wananchi kuwa virusi hivyo haviwezi kusambaa kwa kasi kama ilivyokuwa kwa ugonjwa wa COVID-19.
Akizungumza Ijumaa mjini Geneva, msemaji wa WHO, Christian Lindmeier, amesema hatari ya virusi hivyo kuenea kwa jamii kwa ujumla bado ni ndogo sana licha ya taharuki iliyotanda baada ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa WHO, hadi sasa watu wanane wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo, huku watatu wakifariki dunia. Vipimo vya maabara vimebaini kuwa wagonjwa hao waliambukizwa aina nadra ya virusi vya Andes, vinavyopatikana zaidi nchini Argentina.
Virusi hivyo viligundulika ndani ya meli ya MV Hondius iliyokuwa katika safari ya kitalii kabla ya kulazimika kutia nanga nchini Cabo Verde kwa ajili ya hatua za kitabibu. Kwa sasa, meli hiyo inaelekea visiwa vya Canary barani Ulaya huku mamlaka za afya zikiendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu.
WHO imeeleza kuwa tofauti na COVID-19, virusi vya Hanta haviambukizwi kwa urahisi kupitia mawasiliano ya kawaida. Shirika hilo limesema maambukizi hutokea zaidi kwa watu wanaokuwa karibu kwa muda mrefu na mgonjwa, ikiwemo wanafamilia, wapenzi au wahudumu wa afya.
“Baadhi ya watu waliokuwa wakikaa vyumba vya pamoja ndani ya meli hiyo hawakuambukizwa, jambo linaloonyesha kuwa virusi hivi haviambukizwi kirahisi,” amesema Lindmeier.
Shirika hilo pia limebainisha kuwa mhudumu mmoja wa ndege kutoka Uholanzi aliyewahi kuwasiliana kwa muda mfupi na mmoja wa wagonjwa waliokufa alipimwa na kukutwa hana maambukizi.
Kwa mujibu wa WHO, mgonjwa wa kwanza alianza kuonyesha dalili Aprili 6, 2026 akiwa ndani ya meli hiyo kabla ya kufariki. Mke wake naye aliambukizwa na baadaye kufariki dunia baada ya kuhamishiwa Afrika Kusini kwa matibabu.
Imeelezwa kuwa kabla ya kupanda meli hiyo, wawili hao walikuwa wametembelea Argentina, Chile na Uruguay katika safari ya kutazama ndege pori kwenye maeneo yenye panya wanaobeba virusi hivyo.
WHO imesema hakuna abiria wala wafanyakazi waliobaki ndani ya meli wanaoonyesha dalili za maambukizi kwa sasa, huku hatua za kuwafuatilia wote waliowahi kuwasiliana na wagonjwa hao zikiendelea kupitia taarifa za safari za ndege, meli na maeneo waliyotembelea.
Operesheni hiyo inasimamiwa chini ya Kanuni za Kimataifa za Afya (IHR), ambapo WHO inashirikiana na mamlaka za afya za Hispania, Uingereza, Argentina, Afrika Kusini pamoja na Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa ili kuhakikisha mlipuko huo unadhibitiwa mapema.


