NEW YORK, Marekani
TAASISI ya Tafiti za Amani ya Stockholm nchini Sweden (SIPRI) imebaini kuwa manunuzi ya silaha za kivita duniani yamekuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea.
Katika utafiti wake, SIPRI imebaini kuwa manunuzi ya silaha yaligharimu Dola za Marekani trilioni 2.887 mwaka 2025.
Kiwango hicho kikubwa zaidi kuwahi kutumika, kilielezwa katika manunuzi ya meli za kivita, ndege, na silaha singine, zikiwamo bunduki.
Bara la Ulaya, kwa mujibu wa utafiti, ndilo lililoongoza kwa manunuzi makubwa, likishuhudia ongezeko la asilimia 14 na kufikia Dola bilioni 864.
Ujerumani iliongeza kwa asilimia 24 bajeti yake ya Wizara ya Ulinzi mwaka 2025, wakati Hispania ilikuwa asilimia 50, huku Poland ikiwa ni asilimia 23.
Xiao Liang ni Mtafiti wa Matumizi ya Kijeshi na Programu za Uzalishaji wa Silaha wa Taasisi ya SIPRI. Anasema: “Ongezeko hilo la matumizi ya fedha nyingi katika ununuzi wa silaha linatokana na vita zinazoendelea, migogoro na sintofahamu za kisiasa zilizopo.”
Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwishoni mwa mwaka 202, mataifa ya Ulaya yamekuwa na mtazamo wa kujilinda zaidi, kwa mujibu wa Xiao.
Kwa mwaka 2025, dunia iliendelea kushuhudia vita kati ya Urusi na Ukraine, wakati huo pia Israel na Humas wakiendelea kushambuliana katika Ukanda wa Gaza.
“Kama ambavyo tumeona vita hivyo vikiendelea na mataifa mengi kutumia fedha nyingi kununua silaha, tutegemee hali kuwa mbaya zaidi,” amesema Xiao.
Wakati huo huo, kwa mwaka 2025, Marekani ilikuwa na matumizi madogo, ikitumia Dola bilioni 954 pekee, pungufu ya asilimia 7.5 ukilinganisha na mwaka 2024.
Kwanini? Hiyo ilitokana na uamuzi wa Bunge kuizuia Serikali kuisaidia Ukraine kama ilivyokuwa imefanya kwa miaka mitatu mfululizo.
Lakini, huenda safari hii matumizi yakaongezeka mara dufu baada ya Marekani kushambulia Iran. Siku sita tu za mwanzo wa vita hiyo iliyoanza Februari 28, 2026, Marekani ilitumia Dola bilioni 11.3.


