CAIRO, Misri
WIKI sita za vita kati ya Marekani na Israel zinazoishambulia Iran imesababisha mtikisiko mkubwa katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika. Makala haya yanachambua zaidi.
Ikumbukwe, vita vimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta, hivyo mashirika ya ndege kulazimika kupandisha bei ya tiketi.
Taarifa zinaeleza kuwa katika baadhi ya masoko, bei ya mafuta ya ndege imepanda hadi mara mbili.
Kupanda kwa bei ya mafuta kulitokana na hatua ya Iran kuufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha asilimia 20 ya rasilimali hiyo.
Mbali ya bei ya mafuta, hali mbaya ya usalama huko Mashariki ya Kati imesababisha baadhi ya mashirika kusitisha safari zake katika maeneo hayo.
Shirika la Ndege la Kenya ni miongoni mwa yaliyochukua hatua hiyo, na badala yake linaelekeza nguvu kubwa katika safari za Ulaya.
Itakumbukwa, Shirika la Ndege la Ethiopia lilitangaza kupata hasara ya Pauni milioni 137 katika kila wiki ya vita hivyo.
“Shirika limesitisha safari zake zaidi ya 100 kwa wiki. Katika baadhi ya safari, tungeweza kupeleka hata ndege tatu kwa siku. Tumepoteza takribani Pauni milioni 137 kwa wiki,” alisema Meneja wa Biashara wa Shirika hilo, Lemma Yadhecha.
Akizungumza hali hiyo, Dominick Andoh, ambaye ni mmiliki wa jukwaa la kidigitali la habari za anga la AviationGhana, anasema:
“Mzigo mzito umewaangukia abiria wa usafiri wa anga. Bei ya tiketi imepanda mara dufu kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.”
Katika Mkutano wa Uchumi uliofanyika mjini Washington hivi karibuni, mfanyabiashara maarufu barani Afrika, Aliko Dangote, alisema mashirika mengi ya ndege yanaweza kufa endapo vita hivyo havitokoma.
Kwa upande mwingine, mtikisiko huo wa sekta ya usafiri wa anga umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za utalii barani Afrika.
Emraan Roode ni mtembeza watalii mkazi wa Cape Town, Afrika Kusini, na hapa anazungumzia namna vita vya Iran na Marekani vilivyoitikisa sekta ya utalii nchini humo.
“Mji wa Cape Town ni miongoni mwa maeneo mazuri yanayovuta watalii wengi kuja kutembelea. Vita vimesababisha hali iwe mbaya. Cape Town iko hoi, watembeza watalii na kampuni za utalii zinapitia wakati mgumu,” amesema Roode.
Roode anasikitika kuwakosa watalii wake wa kimataifa waliokuwa wakimpatia kiasi kizuri cha fedha kila walipoingia Cape Town.
“Nimepoteza kati ya Dola 21,000 hadi Dola 30,000 kwa miezi michache ya vita vya Mashariki ya Kati. Vimeathiri biashara yangu, kwa sababu watalii wangu hawana mpango wa kusafiri kutokana na sintofahamu iliyopo,” anasema.


