9.5 C
New York

Siku ya Kimataifa ya kuthamini Popo yaadhimishwa, Tanzania yaaswa kuwalinda

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
APRILI 17, ya kila mwaka Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuthamini Popo, huku wadau wa mazingira wakisisitiza umuhimu wa kulinda viumbe hao wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi wa ikolojia na uchumi wa kilimo.

Wataalamu wa mazingira wanasema licha ya popo kuhusishwa na imani potofu na hofu katika baadhi ya jamii, ukweli ni kwamba viumbe hao ni muhimu katika kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao, kusambaza mbegu na kuchavusha mimea.

Inaelezwa kuwa popo mmoja ana uwezo wa kula kati ya wadudu 500 hadi 1,200 kwa usiku mmoja, hali inayosaidia kupunguza matumizi ya viuadudu vya kemikali. Aidha, popo wanaokula matunda na nekta huchangia katika kurejesha misitu na kuchavusha mazao ya biashara kama korosho, kahawa, kakao, migomba na pamba.

Kwa mujibu wa takwimu za wataalamu, Tanzania ina takriban aina 80 za popo, wakiwemo African Straw-coloured Fruit Bat, wanaojulikana kwa kufanya uhamaji wa umbali mrefu na kusaidia kusambaza mbegu za miti katika maeneo mbalimbali ya misitu.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa idadi ya popo inapungua kutokana na uharibifu wa makazi yao, ukataji miti na matumizi ya kemikali katika kilimo. Baadhi ya aina, ikiwemo Tanzanian woolly bat na Hildegarde’s tomb bat, tayari zimetajwa kuwa katika hatari ya kutoweka.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa viumbe hao, Peter Knights wa Wild Africa amesema popo ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia na wanapaswa kulindwa badala ya kuogopwa.

“Popo ni washirika wetu, si maadui zetu. Wanachangia kwa kiasi kikubwa katika afya ya mazingira na uchumi wetu. Ni wajibu wetu kuhakikisha wanahifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.

Aidha, wadau wa mazingira wamewataka wananchi kuachana na imani potofu zinazowahusisha popo na mikosi au hatari zisizo na msingi wa kisayansi, wakisisitiza kuwa hatari ya kusambaza magonjwa ni ndogo iwapo viumbe hao hawatasumbuliwa.

Katika maadhimisho ya siku hii, jamii imehimizwa kushiriki katika juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kulinda makazi ya popo na kusambaza taarifa sahihi kuhusu umuhimu wao.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img