Na Wakili Baraka Asajile Gwakabale
SHERIA ya Tanzania haitambui kila kifo cha mtoto tumboni kama murder. Ili kosa la murder lisimame, lazima marehemu awe ametambulika kisheria kama mtu aliyezaliwa hai. Hapo ndipo kifungu cha 204 kinaingia.
Kifungu cha 204 kinaeleza kwamba mtoto anatambulika kama mtu pale ambapo amezaliwa hai, hata kama ni kwa muda mfupi, na baada ya kuzaliwa, kitendo cha mtu kikasababisha kifo chake. Hapo, kama nia ovu itathibitishwa, murder inaweza kusimama.

Lakini vipi kama mtoto hajazaliwa? Hapa ndipo kifungu cha 219 kinapotumika. Sheria inatambua kosa la child destruction, si murder.
Kosa hili hutokea pale ambapo mtu anaposababisha kifo cha mtoto aliyekuwa tumboni, mtoto alikuwa katika hatua ya maendeleo ya kuweza kuzaliwa hai, na kitendo kilifanyika kwa makusudi au kwa uzembe mkubwa.
Hii ina maana moja muhimu sana, kwamba kisheria, mtoto tumboni na mtoto aliyezaliwa hai hawachukuliwi sawa katika makosa ya mauaji.
Mahakama hutazama kwa umakini mkubwa hatua ya ujauzito, ushahidi wa kitabibu kuhusu uwezo wa mtoto kuishi nje ya tumbo, nia ya mtuhumiwa, na mazingira ya tukio.
Ndiyo maana katika mashtaka ya aina hii, ushahidi wa madaktari bingwa huwa msingi mkuu wa kesi.
Sheria inalinda uhai, lakini inalinda pia kanuni za uwazi na mipaka ya uwajibikaji wa jinai. Kifo cha mtoto tumboni hakijirushi moja kwa moja kwenye murder. Kila kesi hupimwa kwa vigezo vya kifungu husika.
Ikumbukwe, muda kati ya jeraha na kifo una umuhimu. Hiki ni kifungu ambacho watu wengi hawakijui, lakini kina nguvu kubwa sana katika kesi za murder.
Sheria haishughulikii tu nani alisababisha jeraha, bali pia ni kwa muda gani kifo kilifuata jeraha hilo.
Kifungu cha 205 kinaweka kanuni ya kisheria kwamba, ili mtu awajibike kwa murder, kifo lazima kitokee ndani ya muda uliotambuliwa na sheria tangu jeraha lisababishwe. Huu ndiyo unaoitwa year and a day rule katika tafsiri ya kisheria.
Maana yake ni nini kwa vitendo? Ni kwamba mahakama lazima ijiridhishe kuwa jeraha lililosababishwa ndilo chanzo kikuu cha kifo, hakuna sababu mpya iliyoingia baadaye kukatiza uhusiano huo, na kifo kilitokea ndani ya muda unaoruhusiwa kisheria.
Iwapo mtu alijeruhiwa, akaishi kwa muda mrefu, na baadaye akafariki kwa sababu nyingine tofauti, basi uwajibikaji wa murder unakuwa na mashaka makubwa. Hapa ndipo upande wa mashtaka unapobeba mzigo mzito wa ushahidi.
Mahakama hutegemea sana ushahidi wa kitabibu, ripoti za madaktari bingwa, na maelezo ya maendeleo ya afya ya marehemu tangu jeraha litokee hadi kifo.
Sheria inalenga kulinda kanuni ya haki. Haikubali mtu ahukumiwe kwa murder endapo uhusiano kati ya kitendo chake na kifo umepotea kwa sababu ya muda au sababu mpya.
Katika kesi za mauaji (murder), muda si jambo dogo. Jeraha na kifo lazima viunganishwe kwa sababu na kwa wakati. Ukivunja muunganiko huo, kesi ya murder inadhoofika kisheria.
Mwisho, kesi za mauaji haziendeshwi kwa mihemko. Huamuliwa kwa tafsiri sahihi ya vifungu, ushahidi, na uthibitisho wa nia. Hapa ndipo taaluma ya sheria inapopimwa.
Mawasiliano: – 0784745645


