Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI imeziagiza menejimenti za viwanda mkoani Pwani kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ili kuongeza uzalishaji wenye tija na endelevu.
Agizo hilo limetolewa juzi na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Rahma Kisuo, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa sheria za kazi, ikiwemo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, katika maeneo mbalimbali ya kazi Wilayani Kibaha.
Akizungumza katika viwanda alivyotembelea, alisema ingawa baadhi ya viwanda vinafanya vizuri katika uzalishaji na utekelezaji wa sheria za kazi, bado kuna kasoro ndogo ndogo zinazohitaji kurekebishwa ili kulinda haki na usalama wa wafanyakazi.

“Tumetembelea baadhi ya maeneo ya kazi na kujionea hali ilivyo. Kwa ujumla wanafanya vizuri, lakini kuna mapungufu machache tuliyobaini ikiwemo baadhi ya wafanyakazi kutokuwa na mikataba ya ajira na kutokidhi baadhi ya viwango vya usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Kisuo.
Amewaagiza watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mamlaka za udhibiti kufanya ukaguzi wa kina katika viwanda hivyo ili kutoa ushauri wa maboresho yanayohitajika kwa wawekezaji.
Aidha, amewapongeza wamiliki wa viwanda kwa mchango wao katika kukuza uchumi wa taifa kupitia ulipaji wa kodi na uanzishaji wa ajira kwa Watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, aliyeshiriki katika ziara hiyo, alisema ukaguzi wa awali umebaini changamoto kadhaa katika mifumo ya usalama na afya kazini.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mazingira ya kazi yenye joto kali, vumbi la makaa ya mawe kutapakaa katika maeneo ya kazi, upungufu wa vifaa kinga pamoja na ukosefu wa alama za tahadhari za usalama.
Mwenda amemhakikishia Naibu Waziri kuwa wataalamu wa OSHA watashirikiana na mamlaka nyingine kufanya ukaguzi wa kina ili wawekezaji wapate ushauri utakaosaidia kuboresha mazingira ya kazi na uzalishaji.
Kwa upande wao, viongozi wa viwanda vilivyotembelewa akiwemo Msimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa GF Vehicle Assemblies Ltd, Jacob Lerise, wamemshukuru Naibu Waziri kwa ziara hiyo na kuahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa.
Katika ziara hiyo ya siku mbili Wilayani Kibaha, Kisuo alitembelea viwanda vya Keds Tanzania Co. Ltd, Aluminium Trailers Ltd, GF Vehicle Assemblies Ltd pamoja na Creative Intertraders Ltd.


