KIGALI, Rwanda
ILIKUWA ni Januari, 2020, ambapo akiwa anatoka saluni katika mitaa ya mjini Kigali, Janvier Igabe alikutana na mwanadada Josiane Tuyishimire.
Baada ya mazungumzo, walikubaliana kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, ingawa Tuyishimire alimuweka wazi Igabe kuwa ni mwathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.
“Hakunificha, aliniambia juu ya hali yake, niliogopa. Sikuwa nikifahamu sana kuhusu Ukimwi na sikuwahi kuwa na mtu wa karibu anayeishi na ugonjwa huo.
“Lakini nilishataka kuishi naye kwa maisha yangu yote. Kwa kweli, nilimpenda. Alionekana mkarimu na mrembo sana,” anasema Igabe.
Maisha kabla ya ndoa

Tuyishimire anasimulia maisha magumu aliyopitia kabla ya kukutana na Igabe, akisema: “Nilipata maambukizi nikiwa na umri wa miaka saba baada ya kubakwa na baba yake.
“Nilikuwa naishi naye baada ya kuacha wanawake watatu tofauti. Sikujua kama nimeambukizwa hadi nipokuwa na miaka 16.”
Anafichua kuwa baada ya kubaini hali yake hiyo, aliamua kuondoka nyumbani na kwenda kuishi kwa rafiki yake. “Nilipoteza tumaini la kuishi. Maisha yangu yakawa magumu.
“Nilianza matibabu mwaka 2014 lakini nikaacha mwaka 2018. Nilikuwa kwenye msongo wa mawazo, na nilijaribu kujiua mara tatu,” anasema.
Mwaka 2019, ndipo Tuyishimire alipokutana na Taasisi ya Ndineza ya mwanamuziki maarufu wa Injili, Aline Gahongayire, ambayo ilimsaidia kurejea kwenye matibabu. “Mwaka uliofuata, ndipo nikakutana na Igabe,” anasimulia.
Maisha ya ndoa
Baada ya kufunga ndoa mwaka 2021, walifanya uamuzi mgumu wa kujitangaza kupitia mtandao wa kijamii wa YouTube.
Kupitia mitandao, walionesha kiu yao ya kutaka kujua namna ya kuishi kama wanandoa wenye hali tofauti (mmoja mwenye Ukimwi) wanavyoweza kuishi pasi na kuambukizana.
Hata hivyo, kwa Igabe haikuwa rahisi kwani si tu ndugu na marafiki, bali pia jamii kwa ujumla ilimshangaa kwa uamuzi wake wa kuishi na mwanamke mwenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Hatimaye, kupitia mitandao, walikutana na Mtandao wa Watu Wanaoishi na Ugonjwa huo nchini Rwanda (RRP+), ambayo iliwapatia madaktari kwa ajili ya semina ya kuishi bila Igabe kupata maambukizi.
“Jambo la kwanza walilosisitiza madaktari ni nidhamu. Mke wangu anatakiwa kutumia vidonge vya ARVs kila siku … Pia, na mimi natakiwa kutumia dawa za kujikinga,” anasema Igabe.
Baada ya mwezi mmoja tu wa kufuata maelekezo, Tuyishimire mwenye umri wa miaka 29, anasema walianza kufurahia maisha.
“Daktari aliniambia afya yangu imeimarika na sasa tunaweza kufanya mapenzi bila kinga na hata kupata watoto.”
Kwa sasa, Ibage ambaye ni mhandisi ni baba wa watoto wawili, mmoja wa kike akiwa na umri wa miaka minne na mwingine ana miaka miwili, wote wakiwa hawana maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
“Watoto wetu wana afya nzuri, mke wangu anaendelea na dawa zake za ARVs na mimi pia naenda kwenye vipimo kila baada ya miezi mitatu. Tunaishi maisha ya kawaida tu,” anasema Igabe.
Licha ya majukumu ya familia, wanandoa hao ni mabalozi wa vijana ndani ya RRP+, ambao wamekuwa wakiratibu na kuendesha semina kwa wengine wanaoishi wakiwa na hali tofauti kama wao.
“Tumesaidia wenza nane kufunga ndoa. Uelewa hupunguza hofu. Mtu anapofika kiwango kizuri cha matumizi ya dawa za ARVs, hawezi kuambukiza tena Ukimwi,” anasema Igabe.


