Na mwandishi wetu, Gazetini
ACHANA na tambo za mashabiki, sare ya kutokufungana ndiyo iliyohitimisha dakika 90 za mchezo wa ‘derby’ ya Kariakoo kati ya wenyeji Yanga na Simba.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa New Amaan, Zanzibar umechezwa leo Marchi Mosi, 2026, ukiwa ni wa 11 kwa kila timu msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Matokeo hayo yanaiacha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 29, wakati Wekundu wa Msimbazi wako nafasi ya tatu wakiwa na 24.
Kabla ya kukutana, timu hizo za Kariakoo zilikuwa zimekutana mara 142, huku Yanga ikiongoza kwa kuondoka na ushindi (41), wakati Simba ilitamba mara 58.
Katika mechi hizo 142, Yanga na Simba, klabu zenye upinzani mkubwa zaidi katika soka la Tanzania, zilikuwa zimetoa sare 43.
Yanga na Simba leo saa 2:15 usiku kwenye dimba la Amaan Complex zimecheza mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu wa 2025/26.
Aidha, leo ilikuwa mara ya 38 kwa Simba kutokuruhusu bao (clean sheets) mbele ya Yanga, wakati wenzao ilikuwa mara ya 52.
Wakati huo huo, kwa Ligi Kuu pekee, mechi ya leo ilikuwa ya 112, Simba ikishinda 29 na kufungwa mara 42.
Historia inakumbusha pia, derby ya kwanza kati ya timu hizo ilichezwa Juni 7, 1965, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0, wakati huo Simba ikiitwa Sunderland.
Katika hatua nyingine, bado ushindi mkubwa zaidi kuwahi kupatikana ni ule wa Simba kuifunga Yanga mabao 6-0, mchezo wa Julai 10, 1977.
Kama hiyo haitoshi, derby ya leo imeshindwa kuvunja rekodi ya mkongwe Abdallah ‘King’ Kibaden, ambaye anabaki kuwa mchezaji pekee kufunga ‘hat-trick’ katika mchezo wa derby ya Kariakoo.


