Na mwandishi wetu, Gazetini
KUTOKA mitaani, majukwaani, hadi mbele ya kamera na sasa wamejijengea heshima kubwa kupitia sanaa ya uchekeshaji ndani ya Bongo.
Hata hivyo, wapo wachekeshaji walioamua kushirikiana na kutengeneza ‘pacha’, ambayo mwishowe iliweza kukonga nyoyo za wapenzi wa tamthilia na filamu.
Max v Zembwela
Katika miaka ya 2000, Kikundi cha maigizo cha Kaole kilikuwa na umaarufu mkubwa na miongoni mwa nyota wake tishio wakati huo alikuwa ni Max Makanda.
Max alijenga jina kubwa zaidi alipokuwa akishirikiana na swahiba wake Hillary Daudi ‘Zembwela’, ambao kwa pamoja walitengeneza ‘kombinesheni’ iliyopendwa kupita maigizo yaliyokuwa yakirushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Baadaye Max alifariki kwa kile kilichoelezwa kuwa ni maradhi ya mguu. Hapo ndipo alipoibuka Mkewe kuziba pengo kwa kucheza na Zembwela.
Kingwendu v Bambo
Pacha hii nayo ilikuwa kiboko katika eneo la kuvunja mbavu. Kila alipokuwa Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, basi Dickson Makwaya ‘Bambo’ naye hakukosekana. Ni kupitia tamthilia za Kaole.
Licha ya kwamba ni miaka mingi imepita, bado kombinesheni ya wachekeshaji hao imeendelea kuvutia wengi kila inapopata nafasi ya kutumbuiza katika matamasha mbalimbali hapa nchini.
Senga v Pembe
Ulimboka Mwalulesa, maarufu zaidi kwa jina la ‘Senga’, aliinogesha zaidi kombinesheni hii kwa staili yake ya kutia huruma kila alipokuwa akiingia kwenye vita na Pembe, ambaye jina lake halisi ni Yusuf Kaimu.
Kwa upande wake, Pembe mara zote alikuwa ‘mtata’ na silaha yake kubwa ilikuwa ni rungu, ambalo angekuwa nalo kila alipokwenda.
Joti v Mpoki
Kwa majina halisi, Joti anaitwa Lucas Lazaro Mhuvile, wakati Mpoki ni Silvery Mjuni. Ukweli ni kwamba hii ni miongoni mwa pacha za vichekesho zilizodumu kwenye ‘gemu’ kwa muda mrefu.
Safari yao ilianzia miaka ya 2000, wakati huo wakiwa sehemu ya Kundi la Nyota Ensembles lililokuwa pia na mastaa kibao, wakiwamo Single Mtambalike ‘Richie Richie’ na Raymond Allen ‘Bishanga Bashaija.
Steve Mweusi v Ndaro
Hii ni kombinesheni ya kizazi kipya, ukilinganisha na zilizotajwa, ambazo zilianza sanaa wakati huo mitandao ya kijamii ikiwa haina wafuasi hapa Bongo.
Licha ya uchanga wao kwenye gemu, Steve Moses Musa ‘Steve Mweusi’ na Masatu Ndaro ‘Ndaro’ ni kombinesheni matata ya uchekeshaji na kwa sasa ina wafuasi wengi huko mitandaoni.


