LAGOS, Nigeria
JINA alilopewa na wazazi wake ni David Adedeji Adeleke, ingawa mashabiki wa sanaa ya muziki wanamfahamu kwa jina la Davido.
Tofauti na wanamuziki wengi, mkali huyo wa Afrobeat anatokea familia inayojiweza kiuchumi nchini Nigeria.
Baba yake, Adedeji Adeleke, ni tajiri kupitia biashara kubwa anazofanya, wakati mama yake aitwaye Vero (sasa marehemu) alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu.
Kwa upande wake, Davido alizaliwa Atlanta nchini Marekani, kabla ya kurudi Nigeria akiwa mdogo, ambako alisomeshwa shule ya Kimataifa ya Uingereza mjini Lagos.

Mwaka 2011, Davido alirejea Marekani kujiunga na Chuo Kikuu cha Oakwood kwa masomo ya Usimamizi wa Biashara (Business Administration).
Hata hivyo, kwa kuwa ndoto yake ilikuwa kwenye soko la muziki, hakuweza kumaliza masomo. Aliacha chuo na kujikita kwenye muziki.
Hesabu zake ziliitika baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza uitwao ‘Back When’ aliomshirikisha rapa wa Nigeria, Naeto C.
Licha ya kuanza kukubalika, ngoma iliyomtoa moja kwa moja na kuingia kwenye orodha ya mastaa wa muziki ni ‘Dami Duro’ aliyoachia mwaka 2011.
Mwaka 2012, aliingiza sokoni Albamu yake ya kwanza, ‘Omo Baba Olowo’, ambayo tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili ni ‘Mtoto wa Tajiri’.
Katika albamu hiyo, kuna nyimbo kali zilizoteka vituo vya redio na runinga vya ndani na nje ya Nigeria. Miongoni mwa hizo ni ‘Ekuro’, ‘Gbon Gbon’ na ‘All of You’.
Kufikia hapo, Davido akawa mmoja ya wasanii wakubwa, kiasi cha kubeba tuzo za Kora (2013) na BET (2014).
Nje ya kazi, Davido amekuwa mstari wa mbele katika kurudisha kwa jamii. Kutoa sehemu ya fedha zake kwa ajili ya kusaidia wenye mahitaji.
Itakumbukwa alivyochangia zaidi ya Dola za Marekani 600,000 katika vituo vya kulea watoto yatima nchini Nigeria mwaka 2021.


