KAMPALA, Uganda
HALI ya afya ya mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, imeripotiwa kuwa mbaya wakati huu akiendelea kusota gerezani.
Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na Chama chake, PFF, Besigye amekimbizwa katika hospitali moja mjini Kampala kwa ajili ya matibabu akiwa chini ya ulinzi mkali.
Hata hivyo, mamlaka za gereza analoshikiliwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 69 zimekanusha madai hayo na kusema alipelekwa kukutana na daktari wake na ni utaratibu wa kawaida.
Besigye, ambaye ni daktari wa zamani wa Rais Yoweri Museveni kwa sasa ni mpinzani mkubwa wa kiongozi huyo na amekuwa gerezani tangu Novemba, 2024.
Anashitakiwa kwa makosa ya uhaini, kumiliki silaha kinyume cha sheria na kutishia usalama wa taifa. Endapo atakutwa na hatia, atahukumiwa kifo.
Wachambuzi wa siasa za Uganda wanakumbuka kuwa Besigye amekwaana na Museveni mara nne katika kinyang’anyiro cha urais.
Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ya Uganda ilimnyima dhamana, ikiwa ni kwa mara ya nne chombo hicho kimetupilia mbali ombi lake hilo.


