MAPUTO, Msumbiji
JINA lake ni Rosita Salvador Mabuiango lakini wengi nchini Msumbiji wanamwita ‘Mtoto wa Muujiza’ kutokana na alivyozaliwa wakati mama yake akiwa juu ya mti.
Mwanzoni mwa mwaka 2000, Msumbiji ilikumbwa na mafuriko yaliyosababisha vifo vya mamia ya raia na maelfu wakilazimika kuyakimbia makazi yao.
Taarifa zilieleza kuwa chanzo cha mafuriko hayo makubwa zaidi kuwahi kutokea ni kufurika kwa Mto Limpopo huko Kusini mwa nchi hiyo.
Katika kujiokoa, mwanamke mjamzito aitwaye Carolina Cecilia Chirindza alikwea juu ya mti, kabla ya kujifungua mtoto wa kike (Rosita) na kisha kuja kuokolewa na helikopta ya Serikali.
Sasa, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Rosita amefariki akiwa na umri wa miaka 25 baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
Miongoni mwa waliojitokeza kumlilia Rosita ni Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, ambaye amemtaja kuwa ni alama ya wasichana nchini humo.


