Na mwandishi wetu, Gazetini
MIMBA zisizotarajiwa ni janga linalopuuzwa, licha ya ukubwa wake duniani kote, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya uzazi na haki za kijinsia (UNFPA).
Kupitia programu yake ya ‘Seeing the Unseen’, UNFPA inaeleza kuwa mimba zisizotarajiwa zaidi milioni 121 hutokea kila mwaka duniani.
Ni wastani wa mimba 331,000 kwa siku, huku ripoti ya UNFPA ikitahadharisha kuwa idadi inaweza kuongezeka zaidi endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa.
“Uwezo wa kuamua kuwa na watoto, idadi ya watoto wa kuwa nao ni haki ya msichana na mwanamke,” inaeleza ripoti hiyo ya mwaka 2022.
“Inapotokea haki hiyo kupuuzwa kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo za kijamii au kukosa huduma ya afya, madhara yake yanakuwa makubwa zaidi.”
Ripoti inafichua kuwa mimba tatu kati ya tano zisizotarajiwa huishia kutolewa, licha ya kwamba njia hiyo inayotumiwa na wanawake zaidi ya milioni saba duniani kila mwaka inaweza kusababisha kifo kwa asilimia zaidi ya 45.
UNFPA kupitia ripoti yake inaeleza sababu za mimba zisizotarajiwa kwa wasichana na wanawake wengi duniani.
Kwa mujibu wa UNFPA, wengi hawajafikiwa na elimu sahihi ya matumizi ya njia za kisasa za kuwawezesha kujikinga na mimba zisizotarajiwa.
“Duniani kote, wanawake takribani milioni 257 wanaotaka kuepuka kupata ujauzito bado hawatumii njia za kisasa. Kati ya hao, 172 hawatumii kabisa,” inaeleza ripoti hiyo.
Wakati huo huo, zipo taarifa zilizobeba dhana potofu juu ya njia hizo, kwamba zina madhara kwa mtumiaji.
Ni kutokana na janga la uelewa mdogo, UNFPA imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na mimba zisizotarajiwa.
Baadhi ya hatua si tu kampeni za kutoa elimu, bali pia Shirika hilo lilijitolea kugawa kondomu zaidi ya milioni 724 kwa mwaka 2020 pekee.


