BEIJING, China
MWANAHARAKATI wa demokrasia wa Hong Kong, Jimmy Lai, atahukumiwa kifungo cha maisha gerezani endapo atakutwa na hatia katika mashitaka yanayomkabili.
Lai (78), anashutumiwa kwa kushirikiana na ‘wadau’ wa nje ya Hong Kong kuhamasisha maandamano makubwa ya mwaka 2019.
Bilionea huyo ambaye ni mmiliki wa vyombo vya habari, amekuwa akishikiliwa tangu aliokamatwa Desemba, 2020.
Huku Hong Kong ikidai kuwa Lai anashitakiwa kwa mujibu wa sheria, wapo wanasema tajiri huyo ni muhanga wa jitihada za mamlaka kuwashughulikia wakosoaji.
Familia yake imelalamikia kuzorota kwa afya ya Lai akiwa mahabusu. Kwa mujibu wa mtoto wake, Sebastian, ni kama baba yake anatumikia adhabu ya kifo.

Kwa miaka mingi, Lai amekuwa mkosoaji mzuri wa Serikali ya China, akipaza sauti yake mara kadhaa kulaani uminywaji wa demokrasia.
Licha ya kuzaliwa na wazazi matajiri, Lai alijikuta akiishi maisha magumu baada ya mali za familia kutaifishwa na Serikali ya Kikomunisti iliyoingia madarakani mwaka 1949.
Akiwa na umri wa miaka 12 tu, aliacha familia yake, akitumia usafiri wa boti ya uvuvi kwenda Hong Kong kwa lengo la kutafuta maisha.
Leo hii, maisha magumu siyo stori tena kwa Lai. Ni miongoni mwa mabilionea wakubwa barani Asia. Kando na biashara nyingine, ndiye mmiliki wa jarida maarufu la mtandaoni la Next. Pia, anamiliki Gazeti lenye wasomaji wengi la Apple Daily.


